Home Burudani Mimi Mars avunja ukimya

Mimi Mars avunja ukimya

0

Mwanamuziki na mwigizaji wa Tanzania Mimi Mars amezungumza kwa mara ya kwanza tangu aliporipotiwa kuhusika kwenye ajali mwanzo wa mwaka huu wa 2024.

Alichapisha video jana kwenye akaunti yake ya Instagram ambapo alisema anaendelea kupata nafuu na hivi karibuni atarejelea kwazi zake kama mwanamuziki, mwigizaji na mtangazaji wa bidhaa mitandaoni.

“Hii inaonyesha kwamba ninarudi vizuri kabisa na niko tayari kuanza kazi, tukae karibu na ukurasa wangu ili tuweze kuona mambo mazuri. Waliozoea kuniona kwenye runinga, waliozoea kuniona jukwaani, waliozoea kuniona kwenye tamasha na hata kwa kutangaza bidhaa, kwa kufupi kazi imerudi.” alisema Mars.

Alishukuru wafuasi wake mitandaoni na wapenzi wa kazi zake kwa kumwombea afueni ya haraka na anasema maombi hayo yamemsaidia sana katika safari yake ya kupona.

Mimi Mars ni dadake Vanessa Mdee ambaye pia ni mwanamuziki na mwezi Januari aliripotiwa kuhusika kwenye ajali ya barabarani habari ambazo familia haikuweka wazi.

Vanessa wakati huo aliomba wanamitandao kuheshimu familia yao huku akiwahakikishia kwamba Mars ambaye alilazwa hospitalini kwa muda alikuwa anaendelea kupata nafuu.

Mdee ambaye anaishi Marekani alisafiri hadi Tanzania kumwona dadake hospitalini ambapo alichapisha video fupi iliyoonyesha Mars na wengine.

Website | + posts