Home Habari Kuu Ubabe wa uongozi Kiambu:  Gachagua akutana na Wawakilishi Wadi

Ubabe wa uongozi Kiambu:  Gachagua akutana na Wawakilishi Wadi

0

Naibu Rais Rigathi Gachagua leo Jumatatu alikutana na Wawakilishi Wadi kutoka kaunti ya Kiambu katika makazi yake rasmi mtaani Karen.

Lengo ni kusikiliza kiini cha mivutano ya kila mara kati yao na Gavana wa kaunti hiyo Kimani Wamatangi.

Awali, Wawakilishi Wadi hao walitishia kumtimua Gavana wamatangi, wakimtuhumu kwa miongoni mwa mambo mengine, kuwatenga katika uendeshaji wa masuala ya kaunti hiyo.

“Serikali ya kitaifa ikiongozwa na Rais William Ruto imeingilia kati mzozo baina ya Gavana wa kaunti ya Kiambu Kimani Wamatangi na uongozi wa kitengo cha ugatuzi, ukiongozwa na Wawakilishi Wadi,” alisema Gachagua.

“Leo asubuhi, nimekutana na Wawakilishi Wadi wa kaunti hiyo katika makazi rasmi mtaani karen kusikiliza malalamishi yao kabla ya kukutana na wabunge wao na baadaye Gavana ili kutafuta suluhu ya amani.”

Kulingana na Naibu Rais, utawala wa Rais Ruto unapigia debe ugatuzi thabiti na hautaruhusu kukithiri kwa mivutano inayokwamisha utoaji huduma kwa raia.

Katika kaunti ya Meru, juhudi za Gachagua kupatanisha Gavana Kawira Mwangaza na Wawakilishi Wadi ziligonga mwamba.

Hii ni baada ya Wawakilishi Wadi hao kwa mara ya pili kumtimua Gavana Mwangaza kufuatia kushindwa kwa juhudi za kuzipatanisha pande kinzani.

Gavana Mwangaza atajumua hatima yake wiki hii bunge la Seneti litakapojadili kutimuliwa kwake.

Ikiwa bunge la Seneti litakubaliana na mashtaka ya Wawakilishi Wadi, basi Mwangaza atakuwa Gavana wa kwanza kufurushwa mamlakani baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2022.

Awali, bunge la Seneti lilitibua juhudi za Wawakilishi Wadi kutaka kumtimua Gavana Mwangaza baada ya kupuuzilia mbali mashtaka yote yaliyowasilishwa dhidi yake.

Website | + posts