Home Habari Kuu Miili saba zaidi yafukuliwa Shakahola

Miili saba zaidi yafukuliwa Shakahola

0

Miili saba zaidi imefukuliwa leo Jumanne, katika eneo la Kwa Mugambi kwenye msitu wa Shakahola, kaunti ya Kilifi. 

Kufukuliwa kwa miili hiyo kumeongeza idadi juma la miili iliyofukuliwa kuwa 443, tangu kuanza kwa zoezi hilo ambalo limefika awamu ya tano.

Zoezi hilo linafanywa na maafisa kutoka Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), kwa ushirikiano na asasi zingine za serikali.

Tayari miili 34 ambayo imetambuliwa imekabidhiwa familia yao na serikali.

Zaidi ya miili 400 ilikuwa imehifadhiwa kwenye kontena nje ya hifadhi ya maiti ya Hospitali ya Kaunti Ndogo ya Malindi.

Mauaji hayo yalihusishwa na mafundisho ya mhubiri mwenye utata Paul Mackenzie, ambaye aliongoza Kanisa la Good News International.

Mhubiri huyo na washukiwa wengine 94 kwa sasa wako rumande wakikabiliwa na mashtaka kadhaa yakiwemo mauaji, kuua bila kukusudia, mafundisho ya itikadi kali na kutesa watoto miongoni mwa mengine.

Zoezi la ufukuzi linatarajiwa kudumu hadi pale serikali itakapotoa uamuzi kuhusu hatma ya miili ambayo haijatambuliwa.

Inatarajiwa kwamba miili yote ambayo haijatambuliwa itazikwa katika kaburi la pamoja ndani ya msitu wa shakahola, kulingana na wapelelezi wanaohusika na uchunguzi.

Mnamo siku ya Jumatatu, Mwanapatholojia Mkuu wa serikali Johansen Oduor alisema makaburi 50 yametambuliwa kwa ufukuzi. Awamu ya tano ya ufukuzi huo ulianza siku ya Jumatatu.