Home Kaunti Mifugo walioibwa waendelea kurejeshwa Isiolo

Mifugo walioibwa waendelea kurejeshwa Isiolo

0

Mbuzi 19, ng’ombe wawili na ngamia mmoja waliokuwa wameibwa katika kaunti ya Isiolo wamerejeshwa.

Hii ni baada ya mifugo hao kupatikana katika kaunti ya Samburu.

Makataa ya wiki moja iliyotolewa na Waziri wa Usalama wa Kitaifa Kithure Kindiki kwa viongozi wa kisiasa kuwashawishi wakazi kurejesha kwa hiari mifugo walioibwa katika eneo hilo yamekamilika.

Hata hivyo, wawakilishi wadi kutoka kaunti za Isiolo, Samburu na Laikipia wanatoa wito kwa Waziri Kindiki kurefusha muda wa kurejeshwa kwa mifugo hao.

Wanasema lengo ni kuwawezesha kuzuru maeneo ambayo bado hawajatembelea na kuwashawishi wakazi kurejesha mifugo wote walioibwa kabla ya kuanzishwa kwa operesheni ya usalama.

Wakiwahutubia wanahabari katika eneo la Sere Olipi katika kaunti ya Samburu walikorejeshwa mbuzi 19, ng’ombe wawili na ngamia mmoja, wawakilishi wadi hao wakiongozwa na Kelvin Lemantaan wa wadi ya Waso, kaunti ya Samburu na Peter Losu wa wadi ya Ngaremara kaunti ya Isiolo walisema waliweza tu kufanya makongamano matano ya kushauriana na wakazi.

Walisema wanahitaji muda zaidi ili kutembelea maeneo hayo hasa kutokana na ukubwa wake.

Bruno Mutunga
+ posts