Waziri mpya wa Utalii na Wanyamapori Rebecca Miano, ameahidi kuharakisha mikakati itakayofungua uwezo wa sekta ya Utalii hapa nchini.
Akizungumza leo Jumatano alipokabidhiwa rasmi wizara hiyo na mtangulizi wake Dkt. Alfred Mutua katika makao makuu ya wizara hiyo Jijini Nairobi, Miano alisema ataongoza mashauriano ya kufanyia marekebisho sera za Utalii, ili kushughulikia maswala yanayoibuka kwa lengo la kuchochea ukuaji uchumi wa taifa.
“Nachukua hatamu za uongozi wa wizara hii, wakati taifa hili linaangazia mageuzi ya kiuchumi na kubuni nafasi za ajira,” alisema Miano.
“Lengo langu kuu ni kuchochea ongezeko la mapato ya Utalii ili kuunga mkono ajenda ya maendeleo ya serikali,” aliongeza waziri huyo.
Miano alidokeza kuwa wizara hiyo itashirikiana na wadau wote, kuimarisha uwezo wa sekta hiyo hapa nchini na katika ngazi za kimataifa.
“Nitahimiza utumizi wa teknolojia ya kisasa kuvutia sekta ya usafiri, sio tu kuongeza idadi ya watalii,lakini pia kuweka kumbukumbu ya vivutio vyetu,” alidokeza waziri huyo.
Kwa upande wake Dkt. Mutua ambaye sasa ni waziri wa leba na ulinzi wa jamii, alisema Miano analeta tajriba mpya ambayo itaimarisha mapato katika wizara hiyo.
“Nina hakika Miano ataongeza kasi katika wizara hiyo, hasaa kupitia ushirikiano na serikali za kaunti kuimarisha mapato. Namtakia kila la heri anapoongoza wizara hiyo,” alisema Mutua.
Sekta ya utalii ni yatatu nchini kwa mapato, huku mapato yake yakiwa shilingi Bilioni 352.6 mwaka 2023 ikilinganishwa na shilingi bilioni 268.1 mwaka uliotangulia, hii ikiashiria ukuaji wa asilimia 31.5.