Home Kaunti Mhubiri Mackenzie kuzuiliwa kwa siku saba zaidi

Mhubiri Mackenzie kuzuiliwa kwa siku saba zaidi

Mackenzie na washirika wake walikamatwa mwezi wa Aprili na wanadaiwa kuwaua kwa njaa takriban watu 429.

Mhubiri Paul Mackenzie kuzuiliwa kwa siku saba zaidi.

Mhubiri Paul Mackenzie wa kanisa la Good News International na washtakiwa wenzake 29 wataendelea kuzuiliwa kwa siku saba zaidi, kusubiri uamuzi wa ombi lililowasilishwa upya na serikali mwezi uliopita.

Afisi ya kiongozi wa mashtaka ya umma, iliwasilisha ombi mahakamani kutaka mhubiri huyo pamoja na washtakiwa wenza, kuzuiliwa kwa siku 180 zaidi.

Hakimu mkuu mwandamizi wa mahakama ya Shanzu Yussuf Shikanda, aliwapa mawakili muda wa juma moja zaidi kutathmini ombi hilo na kumfahamisha mteja wao.

Wakati huo huo maafisa wa kutathmini mienendo waliitaka mahakama iwape muda wa siku saba kuwawezesha kukamilisha ripoti za uchunguzi wa kijamii wa jamaa za washukiwa wanaozuiliwa. Kesi hiyo itatajwa tarehe 19 mwezi huu.

Mackenzie na washtakiwa wenzake wanakabiliwa na takriban mashtaka 12 yakiwemo ugaidi, mauaji, kuwafanya watu kujitoa uhai, utekaji nyara, ufundishaji itikadi kali, mauaji ya halaiki, uhalifu dhidi ya binadamu, unyanyasaji wa watoto, udanganyifu na ulanguzi wa pesa.

Mackenzie na washirika wake walikamatwa mwezi wa Aprili na wanadaiwa kuwaua kwa njaa takriban watu 429 kwa ahadi kwamba wangeenda Mbinguni.

Website | + posts
Radio Taifa
+ posts