Home Habari Kuu Mgomo wa madaktari: Rais Ruto atakiwa kuingilia kati

Mgomo wa madaktari: Rais Ruto atakiwa kuingilia kati

0

Makali ya mgomo wa madaktari ulioingia siku ya 20 leo Jumanne yalizidi kuhisiwa katika maeneo mengi ya nchi huku madaktari wakitoa wito kwa Rais William Ruto kuingilia kati na kusuluhisha mzozo huo. 

Akiwahutubia wanahabari, Katibu Mkuu wa Chama cha Madaktari, KPMDU Dkt. Devji Atellah anasema ulipofikia mgomo huo, ni Rais Ruto pekee anayeweza kusuluhisha hali ya vuta ni kuvute kati ya pande husika.

Awali, mazungumzo yaliyoongozwa na Mkuu wa Utumishi wa Umma Felix Koskei kwa dhamira ya kuutafutia ufumbuzi mgomo huo yalishindwa kuzaa matunda.

“Tumekuwa na majadiliano mengi ambapo serikali huja bila mpango wowote,” alilalama Dkt. Atellah.

Aliyasema hayo huku hali ikiwa si hali katika hospitali nyingi za umma ambako wagonjwa walionekana wakielemewa na mzigo wa maumivu wasifahamu madaktari watafika lini kuwahudumia.

Isitoshe katika kaunti ya Kisumu, madaktari walifanya maandamano wakitoa wito kwa serikali kuchukua hatua haraka na kuangazia lalama zao ili kusitisha mgomo huo kwa manufaa ya Wakenya.

 

 

 

Website | + posts