Home Habari Kuu Madaktari mabingwa wajiunga na mgomo, mafunzo ya utabibu UoN yasitishwa

Madaktari mabingwa wajiunga na mgomo, mafunzo ya utabibu UoN yasitishwa

0

Madaktari wote mabingwa kuanzia leo Alhamisi wameazimia kujiunga na mgomo unaoendelea wa madaktari ambao umeingia wiki yake ya tatu na kulemaza huduma katika hospitali za umma. 

Hayo yametangazwa na Katibu Mkuu wa Chama cha Madaktari nchini, KMPDU Dr. Davji Attellah wakati wakiwahutubia wanahabari katika Hospitali ya Rufaa ya Kenyatta leo Alhamisi.

“Kile ambacho hatua hiyo inamaanisha ni kwamba mafunzo ya utabibu katika Chuo Kikuu cha Nairobi, UoN pia yamesitishwa kabisa kuanzia leo hadi ile siku ambayo serikali itasikiliza masuala tuliyoibua katika ilani ya mgomo,” alisema Dkt. Atellah akiwa ameandamana na maafisa wengine wa chama hicho.

Katibu huyo akisisitiza kuwa kamwe hawatarejea kazini hadi Mkataba wa Maelewano (CBA) wa mwaka 2017-2021 utekelezwe kikamilifu kama ilivyokubaliwa awali kati ya chama hicho na serikali.

Miongoni mwa masuala ambayo yameibua utata na yaliyokubaliwa katika mkataba huo ni kutumwa kwa madaktari wanagenzi kuanza kuhudumu katika hospitali mbalimbali nchini.

Ingawa serikali imeridhia kuwatuma madaktari hao, suala tata limegeuka kuwa malipo yao ambayo yamepunguzwa kutoka takriban shilingi 200,000 hadi 47,000.

Madaktari wameapa kuendelea na mgomo wakati ambapo wagonjwa katika hospitali za umma wanaendelea kutaabika wasijue ni lini makubaliano ya kusitisha mgomo huo yatafikiwa na huduma kurejea kama kawaida.

Juhudi za serikali kusitisha mgomo huo hadi kufikia sasa zimeambulia patupu, ikiwa ni pamoja na mazungumzo yaliyoongozwa na Mkuu wa Utumishi wa Umma Felix Koskei.

 

 

 

Website | + posts