Home Habari Kuu Mgomo wa madaktari kuendelea baada ya kukwama kwa mazungumzo

Mgomo wa madaktari kuendelea baada ya kukwama kwa mazungumzo

0

Mgomo wa madaktari ulioingia siku yake ya tisa leo Ijumaa utaendelea hadi masuala yote walioibua yaangaziwe na serikali. 

Hii ni baada ya mkutano ulioandaliwa jana Alhamisi na kuwaleta pamoja wadau mbalimbali ikiwa ni pamoja na Mkuu wa Utumishi wa Umma Felix Koskei, Waziri wa Afya Susan Nakhumicha na maafisa wa chama cha madaktari, KMPDU, miongoni mwa wengine, kukosa kuambulia chochote.

Akiwahutubia wanahabari baada ya kumalizika kwa mkutano huo uliodumu takriban saa nane, Koskei alisema serikali iko tayari kuangazia masuala yaliyoibuliwa na madaktari kwa kuanza na masuala ya dharura.

Hii ni pamoja na suala la kuajiriwa kwa madaktari wanagenzi ambalo limekuwa mojawapo wa sababu kuu za kuitishwa kwa mgomo huo. Koskei akikiri kuwa kulikuwa na hali ya kutoelewa kwa mapana na marefu majukumu ya madaktari hao wanagenzi na kupendekeza wadhifa huo kuangaziwa upya.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa KMPDU Davji Atellah anasema hakuna makubaliano yoyote yaliyoafikiwa kwa masuala 19 walioorodhesha wakati wa mkutano huo, na kwa misingi hiyo, mgomo utaendelea.

Madaktari wanataka mkataba wa maelewano wa mwaka 2017-2021 utekelezwe kikamilifu.

Mkataba huo unaangazia kuajiriwa kwa madaktari wanagenzi na mishahara na marupurupu ya madaktari miongoni mwa masuala mengine.

Madakatri wamepanga kufanya maandamano leo Ijumaa kushikiza matakwa yao.

Mikutano zaidi inatarajiwa kuandaliwa kati ya serikali na madaktari hao ili kutafuta suluhu kwa mgomo huo ambao umelemaza huduma katika hospitali nyingi za umma na kuwasababishia wagonjwa mateso ya kila aina.

Website | + posts