Uhasama umezuka kati ya kinara wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka na Martha Karua wa Narc K miaka mitatu kabla ya kuandaliwa kwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.
Kiini ni nani kati yao anayepaswa kuwa mgombea wa urais wa muungano wa upinzani wa Azimio wakati wa uchaguzi huo.
Viongozi hao wawili wameelezea nia ya kutaka kushika hatamu za uongozi wa nchi na kumbandua Rais William Ruto madarakani.
Sababu ya kila mmoja kujipendekeza kwa wafuasi wa muungano huo ni hatua ya kiongozi wa Azimio Raila Odinga kutangaza kuwa atawania wadhifa wa mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika, AUC.
Raila anakusudia kumrithi Moussa Faki ambaye muda wake wa kuhudumu utakamilika mwezi Februari mwakani.
Wakati Raila akitumai kutwaa wadhifa huo, Kalonzo anasema ni yeye anayestahili kujaza ombwe litakaloachwa na Raila na kuwa mgombea urais wa muungano wa Azimio.
Kalonzo amenukuliwa katika baadhi ya vyombo vya habari akisema Karua bado hana makali ya kutosha kuwania wadhifa huo.
Kwa upande wake, Karua amemtaka Kalonzo kuwa mtulivu mithili ya maji mtungini na kuwawachia wapiga kura wajibu wa kuamua ni nani kati yao anayepaswa kupeperusha bendera ya Azimio kwenye uchaguzi huo.
Hii ni licha ya yaadhi ya wanasiasa wa ODM kunukuliwa wakisema Raila atagombea tena urais wakati wa uchaguzi wa mwaka 2027.
Ikiwa atafanya hivyo, hii itakuwa mara ya sita kwa Raila kujaribu kushindania urais, wadhifa ambao ameutafuta kwa udi na uvumba bila mafanikio.