Home Biashara Mfanyabiashara aliyeripotiwa kutoweka apatikana

Mfanyabiashara aliyeripotiwa kutoweka apatikana

0

Anne Njeri Njoroge mfanyabiashara anayehusishwa na uagizaji wa mafuta ya thamani ya shilingi bilioni 17 amepatikana akiwa sawa jijini mombasa.

Wakili Cliff Ombeta ndiye alitangaza kutoweka kwa mwanamke huyo ambaye ni mteja wake, muda mfupi baada ya kuandikisha taarifa katika afisi za upelelezi wa jinai DCI kuhusu uagizaji huo wa mafuta ambao sasa umeghubikwa na utata.

Ombeta ametangaza tena leo kwamba Njeri amepatikana akiwa sawa jijini Mombasa.

Amefikishwa mahakamani jijini Mombasa kutokana na kile kinachotajwa kuwa kuwasilisha stakabadhi gushi za uagizaji huo wa mafuta.

Wakati alikuwa ametoweka, simu yake ilikuwa imezimwa na maafisa wa polisi wamefafanua kwamba hakuwa amekamatwa nao.

Kampuni mbili Galana Energies Limited na Ramco zinadai umiliki wa shehena hiyo ya mafuta na zimekana kumfahamu Njeri.

Ombeta anasema mteja wake alipata maagizo kutoka mahakama kuu ambayo yanazuia meli hiyo kuondoka na mafuta yasipakuliwe mpaka mzozo wa umiliki utatuliwe.

Bi. Njeri kupitia kwa wakili wake naye anataka mashirika kama shirika linalosimamia bandari nchini KPA, shirika la Kenya Pipeline, shirika la kukusanya ushuru KRA, kampuni za Ramco na Galana ziweke shilingi bilioni 17 kwenye akaunti ya benki inayozalisha faida wanaposubiri kusikilizwa na kuamuliwa kwa kesi hiyo.

Website | + posts