Alice Guo ambaye awali alikuwa meya nchini Ufilipino na ambaye anatuhumiwa kwa kufanyia China upelelezi amekamatwa nchini Indonesia.
Guo amekuwa mafichoni kwa wiki kadhaa na amekuwa akisakwa na maafisa tangu Julai, 2024. Maafisa hao wamekuwa wakimfuatilia kwenye nchi nne.
Analaumiwa kwa kutetea na kulinda kampuni za michezo ya kamari mitandaoni ambazo zilikuwa majukwaa ya ulaghai na ulanguzi wa binadamu katika mji wa Bamban nchini Ufilipino.
Meya huyo wa zamani hata hivyo anakanusha madai yote dhidi yake na kulindana na Rais Ferdinand Marcos Jr wa Ufilipino, Guo anafaa kurejeshwa nchini humo leo Jumatano, Septemba 4, 2024.
Guo alisema alilelewa kwenye shamba la familia yake na kwamba babake mzazi ni raia wa China lakini mamake ni mzaliwa wa Ufilipino. Wabunge waliompeleleza hata hivyo wanasema kwamba alama zake za vidole zinawiana na mzaliwa wa China aitwaye “Guo Hua Ping”.
Wabunge hao wanamlaumu kwa kuwa jasusi na alikuwa anawapa hifadhi wanachama wa magenge ya wahalifu.
Dadake alikamatwa kutokana na kesi yake na kuulizwa maswali na maseneta.
China haijasema lolote kuhusu kesi yake.
Anaaminika kukwepa upekuzi katika mipaka mwezi Julai na kutumia usafiri wa majini kuvuka nchi za Malaysia na Singapore akielekea Indonesia. Jumanne Septemba 3, 2024 alikamatwa kwenye mpaka wa magharibi wa mji wa Jakarta.
Kupitia mitandao ya kijamii, Marcos alisema kwamba kisa cha Guo ni onyo kwa watakaojaribu kukwepa haki nchini humo kwani mkono wa sheria ni mrefu na utawafikia popote.