Home Habari Kuu MCK yabuni jopo la kuandaa miongozo ya vyombo vya habari

MCK yabuni jopo la kuandaa miongozo ya vyombo vya habari

0
Afisa Mtendaji wa MCK, David Omwoyo
Afisa Mtendaji wa MCK, David Omwoyo

Baraza la Vyombo vya Habari Nchini Kenya, MCK limeunda kamati ya kiufundi ambayo imetwikwa jukumu la kuandaa miongozo ya vyombo vya habari kuhusiana na matumizi ya akili bandia, yaani Artificial Intelligence, AI, data na mitandao ya kijamii.

MCK inasema hatua hiyo imetokana na mabadiliko ya kiteknolojia yanayofanyika kwa kasi na kuathiri kwa kiwango kikubwa utendakazi wa vyombo vya habari kote duniani.

Baraza hilo linasema miongozo hiyo inahitajika kwa kusudi la kuhakikisha maadili yanazingatiwa wakati wa matumizi ya AI, data na mitandao ya kijamii katika tasnia ya uanabari nchini Kenya.

Mhariri Mwandamizi wa Idara ya Dijitali ya Shirika la Utangazaji Nchini Kenya, KBC Margaret Kalekye na Silas Kiragu kutoka Idara ya Tekonolojia na Mawasiliano ya shirika hilo ni miongoni mwa wanachama wa kamati hiyo.

Sara Mumbua Nzuki, Michael Michie, Prof. John Walubengo, Susan Mute, Ellen Wanjiru na Carole Kimutai pia wametajwa kama wanachama wa kamati hiyo yenye wanachama 29 itakayohudumu kwa kipindi cha miezi mitatu.

Kamati pia inawajumuisha Michael Oriedo, Dkt. Gilbert Mugeni, Rosemary Mwangi, Demus Kiprono, Oliver Mathenge, Antony Laibuta na Eric Munene miongoni mwa wengine.

“Timu ya kiufundi ambayo inawajumuisha wanachama kutoka nyanja za uanabari, teknolojia, wanazuoni na wanasheria inatarajiwa kuelezea manufaa na matishio ya teknolojia mpya, kutoa mapendekezo ya vigezo muhimu vya kuzingatiwa ambavyo vitasaidia kuboresha ubora wa uanahabari, kujumuisha matumizi ya data katika uandishi wa habari wakati pia ikitoa njia za kitaalam za kuangamiza maudhui mabaya katika vyombo vya habari,” inasema MCK katika taarifa.

“Vyombo vya habari vinatumia AI kuongeza idadi ya wafuasi wake na mrejesho wakati tasnia ya uanahabari ikitafuta njia za kujipatia uumaarufu katika mazingira ya utendakazi yanayobadilika kwa kasi mno,” anaongeza Afisa Mtendaji wa MCK David Mwoyo.

Kamati hiyo inatarajiwa kustawisha nyaraka tatu muhimu ambazo ni Kitabu cha Wanahabari cha Kuripoti kuhusu AI na Data, Miongozo ya Vyombo vya Habari kuhusiana na Matumizi ya AI na Data na Miongozo ya Maadili juu ya matumizi ya Vyombo vya Habari na Intaneti kwa Wanahabari na Mashirika ya Habari.