Home Habari Kuu Mchungaji Dorcas Rigathi aitembelea Israel

Mchungaji Dorcas Rigathi aitembelea Israel

0

Mkewe Naibu Rais, Mchungaji Dorcas Rigathi amefanya ziara nchini Israel ili kukadiria na kujifunza baadhi ya njia bora za kuwarekebisha tabia na kuwatibu waraibu wa pombe na dawa za kulevya.

Alitembelea Malkishua, kijiji kinachofahamika zaidi kwa kuwatibu na kuwarekebisha tabia waraibu wa pombe na dawa za kulevya nchini Israel. Kijiji hicho kinapatikana kwenye mlima Gilboa, ambako Kibiblia, Sauli na watoto wake walifariki na kutoka mlimani hapo, unaweza ukaona vizuri mto Jordan.

Wakati wa ziara hiyo, Mchungaji Dorcas alitangamana kwa saa nyingi na Wanasaikolojia, Washauri, Maprofesa na Matabibu wenye tajiriba ya muda mrefu ya urekebishaji tabia waraibu wa pombe na dawa za kulevya.

Aidha alisikiliza simulizi zilizohadithiwa na waraibu wanaorejea katika hali yao ya kawaida kijijini hapo.

Njia tofauti, rahisi na baadhi ngumu zinatumika wakati wa mchakato wa urekebishaji tabia ambao unajumuisha benchi, utunzaji bustani na utoaji tiba kwa watu binafsi na makundi miongoni mwa njia zingine.

“Dhana ya kijiji inaondoa mtazamo wa kuwa mfungwa, inatoa uhuru, utunzaji na kuhalalisha ndoto. Inaondoa hofu ya kushindwa siku za usoni. Duniani kote, tunakumbana na changamoto sawia lakini kutokana na ubia na ushirikiano, tunaweza tukabadilisha maisha,” alisema mchungaji Dorcas.

Katika kijiji cha vijana cha Yemin Ord katika Mlima Carmel, Dkt.Haim Peri alielezea aina ya elimu inayotumika katika mchakato wa urekebishaji tabia inayowapa waraibu wanaorejelea hali ya kawaida fursa ya kupata elimu katika mandhari ya nyumbani, na kuachana kabisa na uraibu wa kutumia dawa za kulevya.

Ziara hiyo ilikuwa mwaliko maalum kutoka kwa Well-Being International – Global Advisory Group, kundi linaloongozwa na Prof. Yossi Harel-Fisch.

Nchini Israel, raia wote hujiunga na jeshi baada ya kumaliza masomo ya shule ya sekondari ili kulitumikia taifa, isipokuwa wale wenye majitaji maalum kama vile ulemavu.

Mchungaji Dorcas pia ameanzisha mpango wa kuzuia unywaji wa pombe na utumiaji wa dawa za kulevya katika shule ya upili ya Dagoretti kwa kushirikiana na Shirika la Kupambana na Utumiaji wa Dawa za Kulevya Nchini, NACADA.

Website | + posts

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here