Home Habari Kuu Mchungaji Dorcas afungua kambi ya kuwatibu waraibu wa dawa za kulevya Mombasa

Mchungaji Dorcas afungua kambi ya kuwatibu waraibu wa dawa za kulevya Mombasa

0

Mke wa Naibu Rais Mchungaji Dorcas Rigathi amefungua kambi ya utoaji matibabu na urekebishaji tabia ya Miritini katika kaunti ya Mombasa. Kambi hiyo inawalenga waraibu wa pombe na dawa za kulevya mjini Mombasa. 

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kambi hiyo, Mchungaji Dorcas alitoa wito kwa jamii kuhusika katika urekebishaji wa tabia za waraibu hao na kuwakubali katika jamii punde baada ya kutibiwa.

“Ni sharti tuwasaidie waraibu hao kuachana na matumizi ya pombe na dawa za kulevya na kuchukua hatua madhubuti ili kuwaweka kwenye njia sahihi.”

Wakati wa hafla hiyo, Halmashauri ya Bandari Nchini, KRA ilitoa mchango wa shilingi milioni moja kwa mpango wa kuwasaidia watoto wavulana unaoendeshwa na ofisi ya mke wa Naibu Rais.

Kaimu Afisa Mkuu Mtendaji wa hospitali ya Coast General Dkt. Wanjiru-Korir pia aliahidi kushiriki mpango huo.

Wengi wa waraibu walipongeza mpango huo walioutaja kama ule utakaobadilisha dira ya maisha yao.

Juzi Jumatano, Mchungaji Dorcas alifungua kambi ya siku mbili inayowalenga waraibu katika dispensari ya Railways katika eneo la Shimanzi katika kaunti ya Mombasa.

Mkurugenzi wa utiifu wa mamlaka ya kupambana na dawa za kulevya, NACADA James Koskei aliahidi kuwa mamlaka hiyo itaunga mkono mpango huo siyo tu katika eneo la pwani bali kote nchini.

Website | + posts