Home Burudani Mchekeshaji Eric Omondi atangaza kukamilika kwa mradi wa daraja Kisii

Mchekeshaji Eric Omondi atangaza kukamilika kwa mradi wa daraja Kisii

0
kra

Eric Omondi ambaye wengi wanamfahamu kama mchekeshaji ametangaza kukamilika kwa mradi wa daraja ambalo alilipa jina la “Kemunto”.

Jina hilo ni la mtoto mdogo ambaye alionekana akivuka mto Gucha huko Kisii kwa kutumia daraja la awali ambalo lilikuwa bovu na hatari kwa maisha akielekea shuleni.

kra

“Daraja la Kemunto limekamilika. Msichana huyu mdogo amebadilisha maisha ya jamii nzima. Yeye ni shujaa.” aliandika Eric Omondi akiongeza kwamba daraja hilo ni la kihistoria na ishara ya kujitolea kwa umma.

Alisema pia kwamba ni ishara kubwa ya kauli kwamba kuna nguvu katika umoja kwani ujenzi wa daraja hilo ulifanikishwa na michango ya watu mbali mbali, wafuasi wake kwenye mitandao ya kijamii.

Omondi huwa anaendesha michango kupitia akaunti zake za mitandao ya kijamii kusaidia watu mbali mbali wasiobahatika katika jamii, michango aliyoipa jina la “Sisi kwa sisi”.

Anafurahia kwamba wakenya wanaweza kuungana kutatua shida zao, kuziba mianya kati ya matajiri na maskini na kwamba hakuna kisichowezekana katika umoja.

Video ya mtoto Kemunto akivuka mto huo ambao maji yake mengi hutiririka kwa kasi ilisambaa mitandaoni mwezi jana na ilipomfikia Eric, akaamua kuchukua hatua.

Alisafiri hadi Kisii kutafuta mtoto huyo na kufika katika eneo husika. Naye alinakiliwa video akijaribu kutumia daraja hilo hatari na kutoa wito wa michango ya kufanikisha ujenzi wa daraja salama.

Babake msichana huyo ndiye alikuwa akipokea michango hiyo na sasa kazi imekamilika.

Website | + posts