Home Habari Kuu Mbunge wa zamani wa Mandera Kusini asakwa kwa tuhuma za ufisadi

Mbunge wa zamani wa Mandera Kusini asakwa kwa tuhuma za ufisadi

0

Mahakama ya Kupambana na Ufisadi mjini Mombasa imemuamrisha mbunge wa zamani wa Mandera Kusini Adan Haji Ali Sheikh kufika mbele yake ili kujibu mashtaka ya ufisadi yaliyowasilishwa dhidi yake. 

Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi, EACC inasema Haji anakwepa kukamatwa.

Mbunge huyo anasakwa na EACC kujibu mashtaka ya ufisadi dhidi yake yanayohusiana na fedha ambazo kima chake ni shilingi milioni 51.4. Mbunge huyo anadaiwa kutekeleza uovu huo alipohudumu kama Waziri wa Utalii wa kaunti ya Kwale kati ya mwaka 2013 na 2017.

EACC inasema mshukiwa alitumia hoteli yake inayojulikana kama Lotfa Resort Diani Limited kufanya biashara na serikali ya kaunti.

Hoteli hiyo, ambayo wakurugenzi wake walikuwa mke na mtoto wake wa kiume, ilitoa huduma za malazi na mikutano kwa serikali ya kaunti kwa gharama ya juu zaidi.

Aidha mbunge huyo hakufichua kuwa alikuwa na maslahi ya kibinafsi wakati wa utoaji zabuni na hivyo kuwa na mgongano wa maslahi kinyume cha sheria.

Mbunge huyo anaaminika kwenda mafichoni baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma mnamo mwezi Disemba mwaka jana kukubaliana na mapendekezo ya EACC ya kumkamata na kumshtaki chini ya Sheria ya Uhalifu wa Kiuchumi ya Mwaka 2023.

Website | + posts