Home Habari Kuu Mbunge wa Magarini Harrison Kombe atupwa nje na mahakama

Mbunge wa Magarini Harrison Kombe atupwa nje na mahakama

0

Mbunge wa Magarini Harrison Garama Kombe amepoteza kiti chake cha ubunge, baada ya Mahakama ya Upeo kutupilia mbali uchaguzi wake.

Jopo la majaji watano katika Mahakama ya Upeo lilithibitisha matokeo ya Mahakama ya Rufaa na kuthibitisha madai ya mlalamishi Stanley Kenga Karisa ya kukiuka taratibu za uchaguzi.

Majaji hao waliamuru kwamba IEBC itangaze kiti cha eneo bunge la Magarini kuwa wazi mara moja na kuendelea na uchaguzi mdogo kwa mujibu wa sheria.

Karisa aliwania kiti hicho chini ya chama cha United Democratic Alliance (UDA) katika uchaguzi mkuu wa 2022 dhidi ya Kombe wa Orange Democratic Movement (ODM).

Kombe alimshinda Karisa kwa kura 21 pekee, akipata kura 11,946 dhidi ya 11,925 za Karisa 11,925 .

Hata hivyo, Karisa alienda mahakamani akilalamikia udanganyifu katika uchaguzi huo.

Jaji wa Mahakama kuu Alfred Mabeya alitupilia mbali uchaguzi huo akitaja dosari nyingi ambazo zilidhoofisha uadilifu wa mchakato wa uchaguzi.

Kombe alipinga uamuzi wa mahakama hiyo na kuelekea Mahakama ya Rufaa ambapo alipata pigo kwa mahakama hiyo kudumisha uamuzi wa Mahakama ya kuu.

Kwa mara nyingine Kombe hakuridhishwa na uamuzi huo na kuelekea Mahakama ya Upeo ambapo uchaguzi wake ulibatilishwa.