Home Habari Kuu Mbunge Peter Salasya aomba msamaha

Mbunge Peter Salasya aomba msamaha

0

Mbunge wa eneo la Mumias Mashariki Peter Salasya ameomba msamaha kufuatia kitendo chake cha kumzaba mwakilishi wadi kofi.

Taarifa fupi ya kuomba msamaha ilipachikwa kwenye akaunti ya mtandao wa X yenye jina la kiongozi huyo ambapo aliandika, “Mimi Peter Salasya ningependa kuomba msamaha kwa watu wa Mumias Mashariki na Wakenya kwa jumla.”

Aliendelea kusema kwamba matendo yake katika siku za hivi majuzi hayafanani ya mtu wa hadhi yake anayefaa kuigwa na vijana.

Salasya aliahidi kujitahidi kudhibiti hasira zake kuanzia sasa huku akilaumu shetani kwa yaliyotokea.

 

Video ilisambazwa kwenye mitandao ya kijamii ikimwonyesha Salasya aliyekuwa akihutubia mkutano wa mazishi akimzaba kofi mwakilishi wa wadi ya Malaha-Isongo siku ya Ijumaa.

Mbunge huyo alikamatwa na kulala kwenye seli za kituo cha polisi cha Shianda kwa usiku mmoja na baadaye akaachiliwa kwa dhamana ya pesa taslimu ya shilingi elfu 50.