Home Kimataifa Mbunge Oron aitaka serikali kumaliza mgomo wa matabibu

Mbunge Oron aitaka serikali kumaliza mgomo wa matabibu

0
kra

Mbunge wa Kisumu ya Kati Joshua Oron ametoa wito kwa Wizara ya Afya kutafuta suluhu ya haraka kwa mgomo wa madaktari unaoendelea kote nchini.

Akizungumza katika shule ya upili ya wasichana ya St. Teressa Kibuye, Oron alisema kuwa wagonjwa walikuwa wakitolewa katika hospitali akihofia kwamba huenda maisha yakapotezwa iwapo mgomo huo hautasitishwa haraka.

kra

“Afya ni sekta muhimu sana katika nchi hii na hatuwezi kumudu kucheza nayo. Serikali lazima itafute njia za kumaliza mgomo wa madaktari na kutekeleza malipo yote ya NHIF yaliyowasilishwa na vituo vya afya ili kuhakikisha kuwa hakuna maisha yanayopotezwa katika kipindi hiki,” alisema mbunge huyo.

Oron ambaye alikuwa akifungua bweni katika shule hiyo iliyojengwa kwa ufadhili wa fedha za ustawi wa maeneo bunge, NG-CDF, aliandamana na Mwakilishi wa Wanawake wa kaunti ya Kisumu Ruth Odinga.

Ruth alikashifu serikali kwa shambulio lililofanywa majuzi dhidi ya maafisa wa chama cha madaktari, KMPDU ambao walikuwa wakipigania haki zao.

“Serikali ya Kenya Kwanza lazima iwe na utu, tuna uhuru wa kusema na kujieleza, unyanyasaji huu lazima ukomeshwe,” alisema Mwakilishi huyo wa Wanawake.

Aliongeza kuwa Wakenya wanahitaji madaktari kwa ajili ya huduma zao za afya na kutoa changamoto kwa serikali kupunguza gharama katika safari za ndani na nje ya nchi ili kufadhili sekta hiyo.

Mgomo wa madaktari ulianza saa sita usiku Alhamisi, Machi 14, 2024.

Madaktari wameapa kuwa utaendelea hadi matakwa yao yashughulikiwe.

Alphas Lagat
+ posts