Home Habari Kuu Mbunge Nimrod Mbai alaaniwa kwa kumzaba kofi mfanyakazi wa KPLC

Mbunge Nimrod Mbai alaaniwa kwa kumzaba kofi mfanyakazi wa KPLC

0

Shutuma zinazidi kuongezeka dhidi ya mbunge wa Kitui Mashariki Nimrod Mbai kutokana na hatua yake ya kumzaba kofi mfanyakazi wa kampuni ya umeme nchini, KPLC.

Wa hivi karibuni kusitisha kimya chake kuhusiana na kisa hicho ni kampuni ya KPLC yenyewe.

“Kama kampuni inayotoa kipaumbele kwa maslahi ya wafanyakazi wake na umma, tunalaani kisa hiki na tungependa kuelezea bayana kuwa hatukubali aina yoyote ya vurugu hasa kwa wafanyakazi wetu wakiwa kazini,” ilisema KPLC katika taarifa.

“Tumezitaarifu mamlaka husika juu suala hili ambalo kwa sasa lipo mahakamani.”

KPLC imeahidi kuongeza ufuatiliaji wa mitandao yake na kufanya kazi kwa karibu na maafisa wa serikali ya kitaifa na taasisi zingine za usalama kukabilliana na shughuli zozote zisizokuwa halali.

Kampuni hiyo sasa inatoa wito kwa umma kuripoti visa vyovyote vya uharibifu, uunganishaji wote usiokuwa halali wa umeme na shughuli zingine zozote wanazotilia shaka kwenye mtandao wa umeme kupitia nambari  97771 au kwa mamlaka zilizopo karibu.

KPLC iliyasema hayo wakati Tume ya Kitaifa ya Kutetea Haki za Kibibadamu, KNCHR nayo pia ikizamia suala hilo.

Kwenye taarifa iliyotolewa leo Jumatano, KNCHR ilitoa wito wa kisa hicho kuchunguzwa haraka ili kuhakikisha haki inatendeka.

“Tume inakichukulia kitendo hiki kama ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu na uhuru wa mfanyakazi wa kampuni ya Kenya Power, uvamizi dhidi maadili ya maafisa wa serikali, unaokiuka katiba ya nchi na sheria ya maadili, na uvunjaji wa wazi wa sheria bila kujali ,” alisema mwenyekiti wa KNCHR Roseline Odede.

Tume hiyo kadhalika ilielezea mashaka kuhusiana na madai ya mbunge huyo kutumia bunduki kumtishia mfahanyakazi wa KPLC ambaye alikuwa anatekeleza majukumu yake bila kujihami.

“Kutishia kutumia bunduki, hasa mbele ya raia waliotii sheria ni kitendo cha kizembe zaidi na kinawakilisha ukiukaji mkubwa wa usalama wa umma.”

Mbunge wa Kitui Mashariki Nimrod Mbai tayari amekamatwa na maafisa wa polisi kutokana na hatua yake ya kumzaba kofi afisa wa kampuni ya KPLC.

Mbai alifikishwa mahakani, Kajiado na kuachiliwa kwa dhamana ya shiligu elfu 50 pesa taslimu na atafikishwa tena mahakamani Julai 11.

Taarifa zinaashiria kwamba Mbai, ambaye alinakiliwa kwenye video akitekeleza kitendo hicho, alikamatwa jana Jumanne jioni na alipangiwa kufikishwa mahakamani leo Jumatano huko Kajiado.

Kwenye video hiyo, Mbai alisikika akiamrisha wafanyakazi wa KPLC wawasiliane na wenzao ambao walikuwa wameng’oa na kuchukua vigingi haramu vya kuunganisha umeme.

Kulingana naye, Rais aliagiza kwamba hali kama hiyo inapotokea, KPLC inafaa kulipisha Wakenya na wala sio kukata umeme.

Afisa wa KPLC anaonekana kusalia mtulivu kwenye video hiyo hata baada ya kuzabwa kofi.

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here