Home Kimataifa Mbunge ahukumiwa kifo Congo

Mbunge ahukumiwa kifo Congo

0

Mahakama ya kijeshi nchini DR Congo imemhukumu mbunge Edouard Mwangachuchu adhabu ya kifo kutokana na mchango wake katika maasi ya kundi la M23.

Wakili wa Mwangachuchu ametaja adhabu hiyo kuwa Kali sana na iliyochochewa na ukabila.

Agosti mwaka huu upande wa mashtaka ilikuwa umependekeza kwamba Mwangachuchu wa umri wa miaka 70 ahukumiwe kifungo cha maisha gerezani.

Adhabu ya kifo nchini Congo haijatolewa kwa muda wa miaka 20 sasa na awali waliohukumiwa kifo waliishia kufungwa kifungo cha maisha.

Mwakilishi huyo wa eneo la Masisi katika bunge la kitaifa nchini DRC na ambaye anamiliki kampuni ya kuchimba madini hakuwepo mahakamani wakati wa kusomwa kwa hukumu dhidi yake.

Jaji Robert Kalala alisema kwamba Mwangachuchu alipatikana na hatia ya uhaini, hatia ya kumiliki silaha kinyume cha sheria na kuhusika na maasi ya kundi la M23.

Kundi la M23 limekuwa likitekeleza maasi katika mkoa wa Kivu kaskazini nchini DRC ambapo linadhibiti sehemu kubwa tangu mwaka 2021.

Rwanda Inalaumiwa na Marekani, wataalamu wa Umoja wa Mataifa na Ufaransa kwa kichochea maasi ya kundi la M23. Hata hivyo Rwanda inakanusha.

Mwangachuchu alikamatwa mwezi Machi mwaka huu na kupelekwa kwenye gerezani la Makala jijini Kinshasa na kesi dhidi yake imekuwa ikisikilizwa huko.