Serikali imesema imekamilisha uchunguzi wa mbolea zote zinazosambazwa chini ya mpango wa utoaji mbolea ya gharama nafuu na kuthibitisha kuwa zinaafikia viwango vya ubora vinavyohitajika.
Hata hivyo, serikali imedokeza kuwa baadhi ya mbolea zinatokengenezwa na kusambazwa na kampuni ya KEL Chemical, zimebainishwa kuwa hajizatimiza viwango vya ubora baada ya kufanyiwa uchunguzi na shirika la kukadiria ubora wa bidhaa, KEBS.
Kupitia kwa taarifa leo Ijumaa, serikali imesema kuwa inashikilia mbolea za kampuni hiyo ya KEL Chemicals na imesitisha usambazaji wake katika halmashauri ya taifa ya nafaka na mazao, NCPB.
Aidha, serikali imewashauri wakulima kusitisha matumizi ya mbolea kutoka kwa kampuni ya KEL Chemicals, na kufika katika kituo cha NCPB kilicho karibu kwa maelezo zaidi.
Katika hatua ya kuhakikisha usalama wa umma na kudumisha viwango vya ubora vinavyohitajika, shirika la kukadiria ubora wa bidhaa Kebs limeanzisha hatua za kisheria dhidi ya kampuni ya KEL Chemicals, kwa kusambaza bidhaa za ubora wa kiwango cha chini.
Ilisema aina tatu za mbolea zilizoathiriwa, ambazo ni Kelphos Plus, Kelphos gold na NPK 10:26:10 zilichunguzwa na shirika la ukadiriaji ubora wa bidhaa hapa nchini-KEBS na kubainika kuwa hazijatimiza viwango vya ubora vinavyohitajika.