Home Vipindi Mawe ya dhahabu Rongo? Wakazi wahaha

Mawe ya dhahabu Rongo? Wakazi wahaha

0
kra

Baadhi ya wakazi wa kaunti ndogo ya Rongo wamekita kambi katika eneo la ujenzi wa barabara ndani ya mji wa Rongo kwa siku ya 5 sasa, baada ya kufahamu kwamba baadhi ya mawe yanayotumiwa na kampuni ya ujenzi wa barabara yana chembechembe za dhahabu.

Isitoshe, idadi kubwa ya wakazi hao wameacha kazi nyingine ili kujikita katika kuchota mawe wanayodai kuwa yana dhahabu.

kra

Wanaoendesha vifaa vya ujenzi wa barabara hiyo kama matrekta wamejipata katika hali ngumu ikiwabidi kuwapa nafasi wakazi hao kutafuta chembechembe hizo za dhahabu huku ujenzi wa barabara hiyo ukiendeshwa kwa mwendo wa kinyonga.

Diana Atieno, ambaye amekuwa akifanya kazi katika sekta ya madini ya dhahabu kwa zaidi ya miaka sita, alisema wamebaini kuwa baadhi ya miamba inayotumika katika ujenzi wa barabara hiyo ina mabaki ya dhahabu ambayo kwa sasa inauzwa kwa shilingi 7,200 kwa gramu moja.

Matamshi yake yaliungwa mkono na Tom Ojienda aliyesema kwamba wamebaini kuwa jiwe hilo lina mabaki ya dhahabu na kwa hivyo wako tayari kuyakusanya kadiri wawezavyo ili kupata riziki yao ya kila siku.

Naye Mhandisi wa ujenzi wa barabara hiyo Enos Odum alisema walichukua sampuli ya mwamba huo ili kuufanyia uchunguzi zaidi na kubaini kuwa hakika una mabaki ya dhahabu.

Odum alisema kampuni ya ujenzi imelazimika kufanya kazi kwa pamoja na kuwapa wakazi nafasi ya kutafuta dhahabu.

Alisema wakazi hao wamekuwa na ushirikiano na hivyo wameweza pia kufanya kazi zao za ujenzi ila kwa mwendo wa aste aste.

Celestine Mwango
+ posts