Mawaziri 20 walioteuliwa kuhudumu katika Baraza Jipya la Mawaziri watasailiwa kwa siku nne kuanzia mapema mwezi ujao.
Kwa mujibu wa kamati ya bunge la taifa itakayosimamia usaili huo, mawaziri hao wateule watasailiwa kuanzia Agosti 1 hadi Agosti 4.
Umma una hadi Agosti 1, saa 11 jioni kuwasilisha taarifa yoyote walio nayo kuwahusu mawaziri hao.
Kamati ya bunge itakayoendesha zoezi hilo inatarajiwa kuwasilisha ripoti yake bungeni Agosti 3, ama ikiridhia au kukatalia mbali majina ya walioteuliwa kuhudumu katika wadhifa huo.
Kisha wabunge wataijadili ripoti hiyo na kuiidhinisha au kuikatalia mbali.
Ikiwa majina ya walioteuliwa yataidhinishwa, yatawasilishwa kwa Rais William Ruto kwa uteuzi rasmi.
Watu kadhaa wameteuliwa kuhudumu katika Baraza Jipya la Mawaziri, wakiwemo mawaziri waliohudumu katika Baraza la Mawaziri lililovunjwa.
Wao ni pamoja na Prof. Kithure Kindiki aliyeteuliwa kuhudumu kama Waziri wa Usalama wa Taifa, Aden Duale (Waziri wa Mazingira), Davis Chirchir (Waziri wa Barabara na Uchukuzi), Rebecca Miano (Waziri wa Utalii) na Dkt. Alfred Mutua (Waziri wa Leba).
Viongozi wa upinzani John Mbadi (Waziri wa Fedha), Opiyo Wandayi (Waziri wa Nishati), Wycliffe Oparanya (Waziri wa Vyama vya Ushirika) na Hassan Joho (Waziri wa Madini) pia wameteuliwa kuhudumu katika Baraza Jipya la Mawaziri.