Waziri wa Kilimo na Ustawi wa Mifugo Dkt. Andrew Karanja leo Ijumaa ametembelea ghala za majani chai mjini Mombasa kwa lengo la kutathmini hatua iliyopigwa katika mauzo ya zao hilo.
Kumekuwa na ongezeko la uzalishaji wa majani chai nchini kwa karibu asilimia 30 ikilinganishwa na mwaka jana kutokana na hali nzuri ya hewa na mpango wa mbole ya ruzuku.
Waziri Karanja alitembelea ghala zinazomilikiwa na kampuni ya KTDA Holdings katika miji ya Miritini na Changamwe na pia ghala zilizokodishwa huko Mengo, Mombasa.
Wakati wa ziara hiyo, Waziri aliandamana na mwenyekiti wa kampuni ya KTDA Wilson Muthaura, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Majani Chai nchini Willy Mutai na Mkurugenzi Mkuu wa Huduma za Usimamizi wa KTDA Collins Bett.