Home Habari Kuu Matukio manne yaliozua vilio na mijadala mikali ligi ya EPL 2023

Matukio manne yaliozua vilio na mijadala mikali ligi ya EPL 2023

Ligi kuu ya Uingereza imezua mijadala mingi tangu ujio wa mwamuzi msaidizi wa Video yaani VAR ambao utendaji kazi wake umeleta gumzo kubwa na mtazamo tofauti kutoka kwa wadau mbalimbali wa Soka.

0
Picha za VAR

Mchezo wa kandanda au Soka unahenziwa sana duniani na ndio pekee ulio na mashabiki wengi kote ulimwenguni. 

Japo ligi ya Ujerumani na Uhispania; Bundesliga na Laliga mtawalia zimekuwa na ushindani mkubwa siku za hivi karibuni na vile vile kutoa wachezaji wawili bora duniani, ligi kuu ya Uingereza EPL, imesalia kuwa ligi yenye nguvu zaidi duniani.

Ligi kuu ya Uingereza imezua mijadala mingi tangu ujio wa mwamuzi msaidizi wa Video yaani VAR ambao utendaji kazi wake umeleta gumzo kubwa na mtazamo tofauti kutoka kwa wadau mbalimbali wa Soka.

Mechi 19 za Msimu wa 2023/24 wa EPL zimechezwa kufikia sasa ambapo mwaka umebakisha siku 1 ukamilike, lakini hujakosa matukio si haba! Nusu ya msimu huu umekuwa na matukio mengi kutoka viwanjani hadi vyumba vya kubadilishia nguo;  Nakala hii inakuletea undani wa matukio haya;

MWAMUZI MSAIDIZI WA VIDEO (VAR)

Ni wazi kuwa VAR imeendelea kuleta ufanisi (matokeo chanya) katika michezo mingi pamoja na kukumbwa na changamoto mbalimbali katika baadhi ya mechi.

Kumekuwa na malalamiko katika maamuzi mbalimbali iwe katika Penati, Kuotea, kadi nyekundu na kadi ya njano. VAR inaweza kuathiri karibu kila kipengele cha mchezo.

Lakini je, Hatimaye imekuwa na matokeo chanya au hasi kwenye matokeo ya mechi za Ligi Kuu Uingereza ?

Katika mchezo wa hivi majuzi wa Chelsea dhidi ya Crystal Palace ambapo vijana wa Pochettino waliibuka na ushindi wa mabao 2-1, VAR ilitumika mara zaidi ya 7 na kutatiza mtiririko wa mchezo; wengi wakizua kuelezewa umuhimu wa teknolojia hii ambayo katika dakika ya 89 ilitumika kuizawadi Chelsea Penati katika mojawapo ya matukio yasingehitaji utumiaji wake, jambo ambalo kocha wa Palace Hodgson alielezea kutoridhishwa nalo baada ya mechi hiyo.

La Wiki hii ya Sikukuu ya Krisimasi ilikuwa ni mabishano makali katika kipindi cha kwanza mchezo wa Arsenal na WestHam United wakati Soucek alifunga bao kunako dakika ya 13, na VAR ikashindwa kubaini iwapo mpira ulikuwa umetoka nje kabla ya Jarrod Bowen kucheza mpira wa krosi.

Lililofuatia, Mwamuzi Michael Oliver aliizawadia West Ham bao hilo ambao wengi walisema halingestahili jambo ambalo lilizua mjadala mkali kuhusu iwapo bao hilo lingepaswa kusimama.

Kocha wa Arsenal Mikel Arteta akiongea na waandishi baada ya mchezo huo hakusita kuelezea kughadhabishwa kwake na uamuzi wa VAR.

“Sote tunataka teknolojia bora zaidi ili maamuzi yawe wazi kabisa. Kwa hivyo leo, kama VAR inatoa maamuzi nusu nusu ambayo hayajakamilika na ndio teknolojia tuliyonayo siku hizi, basi ni kitu tunaweza kukiboresha” Arteta alisema akiwa mwingi wa Hasira.

Katika tukio jingine ambalo VAR ilijipata kwa kashfa, ni katika mchezo wa ligi mwezi Novemba 2023 kati ya Chelsea na Tottenham Hotspurs ambapo mashabiki wa soka walishughudia moja ya dakika 45 za kustaajabisha.

Refa akimuonyesha Cristian Romero kadi nyekundu: Picha/Times

Mwamuzi Msaidizi VAR alitumika mara nyingi zaidi katika mechi hii ambapo Spurs ilipoteza wachezaji wake wawili (Christian Romero na Destiny Udogie) walioonyeshwa kadi nyekundu na mabao kukataliwa kwa kuotea; huku kocha wa Spurs Ange Postecoglou akiishtumu VAR kwa kuvua mamlaka ya marefa ambao alihoji kuwa maamuzi mengine hayahitaji VAR.

“VAR Inavua mamlaka ya waamuzi wa michezo, wakati fulani inabidi tukubali maamuzi ya Mwamuzi; hawatakuwa na mamlaka ya kuamua chochote, na tutakuwa chini ya udhibiti wa mtu aliye mbali na ambaye anaona mpira kwa kutazama kiwambo chake (TV)”, alisema Ange Postecoglou Kocha wa Spurs.

Zaidi ya hayo, ukosefu wa usahihi na muingilio wa ushawishi wa VAR katika maamuzi kumejenga taswira ya upendeleo katika vichwa vingi vya wadau wengi wa mitandao na wengi mashabiki wa soka.

EVERTON YAKATWA POINTI 10 KWA KUKIUKA SHERIA ZA FEDHA

Klabu ya Everton ilikatwa pointi 10 katika Ligi Kuu ya Uingereza kwa kosa la kukiuka Kanuni ya Fedha (Faida na Uendelevu), hali ambayo ilitokea katika Msimu wa 2021/22.

Baada ya kutangazwa kwa adhabu hiyo, uongozi wa Klabu ya Everton ulisema utakata rufaa kwa kuwa adhabu hiyo iliwashtua na imekuwa kali licha ya kudai waliwasilisha vielelezo wakati wa mchakato wa kesi hiyo ya ukiukwaji wa Kanuni.

Mshambuliaji wa klabu cha Everton Calvert Lewin: Picha/Everton FC

Kutokana na adhabu hiyo Everton ambayo ilikuwa na pointi 14 wakati huo wa kukatwa pointi hizo na ikishika nafasi ya 14 katika Ligi ilishushwa hadi nafasi ya 19 ikiwa na pointi 4, lakini kwa sasa; Everton inafanya vizuri sana licha ya kupoteza mechi ya juzi dhidi ya City wana alama 16, wakishika nambari ya 17. 

FA KUMSIMAMISHA MSHAMBULIAJI WA BRENTFORD IVAN TONEY

Mwezi Mei mwaka huu wa 2023, mshambuliaji wa Brentford raia wa Uingereza Ivan Toney alifungiwa kucheza soka kwa miezi minane baada ya kupatikana na makosa ya kucheza kamari katika kipindi cha miaka minne.

Ivan Toney: Picha – Mirror

Hata hivyo, katika ripoti za FA hakukuwa na pendekezo kwamba mshambuliaji huyo wa Brentford aliwahi kucheza kamari kwenye timu yake ili ipoteze mchezo.

ADHABU YA FA KWA MANCHESTER CITY

Klabu ya Manchester City inakabiliwa na mashtaka ya chama cha soka nchini Uingereza FA kwa kosa la utovu wa nidhamu kwa wachezaji wake wakati wa mchezo wao dhidi ya Tottenham Hotspurs ambao uliishia sare ya mabao 3-3.

Mchezaji Erling Haaland (kushoto) akimkemea refa Simon Hoper (Kulia) katika dakika ya 94.

Wachezaji wa City na hasaa Erling Haaland alionekana akimpigia makelele refa Simon Hooper baada ya mwamuzi kuinyima Manchester City nafasi ya kushinda dhidi ya Tottenham Hotspur mnamo Desemba 3, 2023.

Mvutano huo ulizidi wakati ambapo Erling Haaland alipomuandalia pasi mshambuliaji Jack Grealish, lakini Hooper akapuliza kipenga, dakika ya 94, na kusimamisha mchezo huku akiashiria kosa la mpira wa Ikabu kwa faida ya City, hali iliyowaghadhabisha wachezaji wa Manchester City kwani walihisi kuonewa.

 

 

 

 

 

Website | + posts