Home Kimataifa Matokeo ya tathmini ya KPSEA yatolewa

Matokeo ya tathmini ya KPSEA yatolewa

Baraza la kitaifa la mtihani hapa nchini-KNEC limetoa matokeo ya mtihani wa kutathmini wanafunzi wa gredi ya sita (KPSEA) wa mwaka-2023.

Wazazi pamoja na wadau wengine, hata hivyo, wataweza kupata matokea hayo kutoka kwa walimu wakuu wao ambao wanaweza kuingia kwenye tovuti ya KNEC.

Maafisa katika baraza la KNEC walithibitisha kwamba matokeo hayo yalichapishwa mtandaoni kufuatia agizo la waziri wa elimu Ezekiel Machogu.

Matokeo hayo yalitolewa siku nne baada ya wanafunzi hao kuripoti katika shule zao siku ya Jumatatu tarehe 15 mwezi huu.

Wanafunzi wa gredi ya sita ambao sasa wameingia gredi ya 7 ndilo kundi la pili kufanya mtihani wa KPSEA chini ya mtaala wa elimu wa CBC.

Machogu aliagiza walimu kuruhusu wanafunzi kujiunga na shule za sekondari msingi kabla ya kutolewa kwa matokeo hayo.

Wanafunzi walioshindwa kununua sare mpya pia waliagizwa kuripoti shuleni na sare zao za gredi ya 6 wanapoendelea na mpito huo wa masomo.

Walimu wakuu pia walihimizwa kutoza karo zinazohitajika pekee na kukoma kuwalazimisha wazazi kugharamia ada za ziada.

Mapema mwezi huu, afisa mkuu mtendaji wa baraza la KNEC David Njeng’ere, alisema usajili wa mtihani wa KPSEA utaanza tarehe 29 mwezi huu hadi mwisho wa mwezi Machi mwaka huu.

Website | + posts
Radio Taifa
+ posts