Mfanyabiashara Nancy Kigunzu Indoveria almaarufu ‘Mathe wa Ngara’ aliyekamatwa siku ya Jumatatu kwa tuhuma za ulanguzi wa dawa za kulevya, amefikishwa mahakamani leo Jumatano.
Hakimu mkuu mwandamizi Njeri Thuku wa mahakama ya uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta, aliagiza Kigunzu azuiliwe kwa siku tano zaidi ili kuruhusu upande wa mashtaka kukamilisha uchunguzi.
Kigunzu aliambia mahakama kuwa anaugua kutokana na msongo wa mawazo na akaomba apewe muda wa kuenda kutibiwa.
Hakimu Thuku alimwelekeza afisa anayesimamia kituo cha polisi cha Muthaiga kuhakikisha kuwa mfanyabiashara huyo anasindikizwa hadi hospitalini kutibiwa.
Katika hati ya kiapo iliyowasilishwa katika mahakama hiyo, idara ya upelelezi wa makosa ya jinai, ilisema kuwa zipo dawa zaidi za kulevya kando na bangi zilizonaswa katika makazi ya Kigunzu, na kuongeza kuwa wanahitaji muda wa kushirikisha wataalam katika kupima na kuchukua sampuli za vyakula vinavyoaminika kusindiliwa bidhaa haramu.