Watu waliopoteza makazi kutokana na mafuriko katika wadi ya Ngaremara, kaunti ya Isiolo wanatoa wito kwa mashirika ya kutoa misaada kupiga jeki juhudi za serikali ya kaunti hiyo kusaidia kuwaondolea mateso.
Familia zisizopungua 1,000 zimelazimishwa kuhama makwao wakati mvua kubwa ikiendelea kunyesha eneo hilo ambalo limeathiriwa mno na mafuriko kutoka nyanda za juu za Isiolo na kaunti jirani ya Meru.
Familia zilizopoteza makazi sasa zimekita kambi katika shule ya upili ya wavulana ya Ngaremara iliyopo nyanda za juu kiasi.
Serikali ya kaunti ya Isiolo inatoa chakula, mahema na mablanketi miongoni mwa bidhaa zingine kwa waathiriwa.
Mwakilishi wadi wa Ngaremara Peter Losu anasema muda umewadia kwa mashirika yasiyokuwa ya serikali kusitisha kwa muda miradi ya maendeleo kama vile uchimbaji wa visima na ujenzi wa madarasa na kuungana na serikali ya kaunti kuwaondolea waathiriwa mafuriko mateso.
Aidha ametoa wito kwa serikali kuu kutoa fedha za dharura kwa serikali za kaunti kuziwezesha kuangazia masaibu ya waliopoteza makwao.
Rais William Ruto kwa sasa anaongoza mkutano wa Baraza la Mawaziri unaotarajiwa kuangazia njia bora za kukabiliana na athari za mafuriko yanayoshuhudiwa katika maeneo mbalimbali nchini.
Serikali kuu imetakiwa kutangaza mafuriko kuwa janga la kitaifa.