Serikali imeshauri mashirika yasiyo ya kiserikali na ambayo hutegemea ufadhili kutoka kwa wahisani na mashirika ya kimataifa kuendesha shughuli zao, yalainishe usimamizi na matumizi ya pesa hizo.
Katibu katika wizara ya mambo ya ndani Daktari Raymond Omollo alitoa taarifa kwa mashirika hayo akisema namna yamekuwa yakisimamia pesa za ufadhili imekuwa ikifaidi nchi ambazo ufadhili unatoka badala ya kuchangia katika ajenda ya kitaifa ya maendeleo na kuelekezwa kwa mambo yanayostahili kupatiwa kipaumbele.
Omollo alisema mfumo ambao wasimamizi wa mashirika yasiyo ya kiserikali wamekuwa wakitumia unaifanya iwe vigumu kwa serikali kusimamia miradi inayotekelezwa na kufanya uangalizi ili kuhakikisha inawiana na maazimio ya nchi na usalama wake.
Katibu huyo alisema Kenya inatambua umuhimu wa ufadhili kutoka nchi nyingine kupitia mashirika hayo lakini kwa sababu ya uwajibikaji, mfumo wa usimamizi wa fedha za mashirika hayo lazima uwiane na mifumo bora inayokubalika duniani kote.
Alisema wameshaandika nyaraka kwa mashirika hayo yasiyo ya kiserikali kuyaelekeza yawianishe mifumo yao na mpango wa serikali wa kiuchumi wa Bottom up.
Omollo alisema pia kwamba serikali inaboresha uwezo wake wa kuchunguza mashirika yasiyo ya kiserikali ili kuhakikisha hayatumiwi kupitisha pesa zisizo halali au zinazokusudiwa kufadhili jinai au ugaidi.