Home Habari Kuu Mashirika ya ajira ughaibuni yalalamikia vikwazo

Mashirika ya ajira ughaibuni yalalamikia vikwazo

0

Mashirika ya kibinafsi ambayo yanahusika na kupeleka wakenya kufanya kazi ughaibuni yamelalamikia vikwazo vilivyopo katika kutekeleza kazi zao nchini Kenya.

Wakizungumza walipokutana na kamati ya bunge kuhusu masuala ya ughaibuni na wafanyakazi wahamiaji inayoongozwa na mbunge wa Taita Taveta Lydia Haika, wawakilishi wa mashirika hayo walisema wanatumia muda mrefu kuwapa mafunzo wakenya hao kabla ya kuwapeleka kufanya kazi ng’ambo.

Walilalamika pia kwamba mamlaka kitaifa ya mafunzo ya kikazi NITA imeweka sharti jipya la kila anayetaka kwenda kufanya kazi ughaibuni kuwa na cheti cha kidato cha nne hatua ambayo imefungia nje wakenya wengi.

Masuala mengine waliyotaja ni ada zilizoongezwa za kupata leseni na mchakato mrefu na ghali wa kupata paspoti za usafiri na stakabadhi nyingine hitajika.

Kaimu mkurugenzi wa uhamiaji wa wafanyakazi Joseph Njue alishukuru kamati hiyo ya bunge kwa kazi inayotekeleza akisema hakufahamu kuhusu mashirika haramu ya kusafirisha wakenya ughaibuni.

Hata hivyo aliahidi kushughulikia malalamishi ya wabunge hao huku akihimiza wakenya kuhakikisha wanatumia mashirika halali kutafuta ajira ughaibuni.

Wakenya wanaweza kudhibitisha uhalali huo kwa kuhakikisha mashirika hayo yamesajiliwa na mamlaka ya ajira nchini NEA.

Tatizo jingine lililoibuliwa wakati wa kikao hicho huko Mombasa ni hatua ya wakenya kukwepa mahala pao pa kazi wanapofika huko suala ambalo linaathiri sifa za mashirika husika.

Haika alihakikishia wawakilishi wa mashirika yanayofanikisha ajira ughaibuni kwamba malalamishi yao yatanakiliwa kwenye ripoti yao.

Website | + posts