Bunge la Seneti kesho Jumatano litaandaa kikao maalum kuangazia mashtaka yaliyosababisha bunge la kaunti ya Meru kumtimua Gavana Kawira Mwangaza kwa mara ya tatu sasa.
Nyaraka zilizotumiwa na wawakilishi wadi kumtimua Gavana Mwangaza tayari zimewasilishwa katika bunge la Seneti kabla ya kuandaliwa kwa kikao hicho.
Wawakilishi wadi 49 kati ya 69 katika bunge la kaunti ya Meru Agosti 8, 2024 walipiga kura kuunga mkono hoja ya kumtimua Gavana Mwangaza madarakani.
Wawakilishi wadi 17 waliipinga hoja hiyo huku watatu wakikosa kupiga kura wakati wa kikao kilichoshuhudia usalama ukiimarishwa maradufu nje na ndani ya majengo ya bunge.
Wakati huu, Mwangaza anakabiliwa na mashtaka ya ukiukaji wa katiba na sheria za kaunti, mienendo mibaya na utumiaji mbaya wa mamlaka yake.
Nadhari sasa ni kwa Bunge la Seneti kuona ikiwa kwa mara nyingine litamnusuru Gavana Mwangaza ambaye amekuwa akilumbana na wawakilishi wadi tangu alipoingia madarakani.
Baadhi ya Maseneta wamenukuliwa wakisema ikizingatiwa malumbano ya mara kwa mara yanayoshuhudiwa katika kaunti ya Meru baina ya viongozi, Rais William Ruto anapaswa kutumia mamlaka yake kuvunja kaunti hiyo ili kupisha uchaguzi mpya.