Kaimu Inspekta Mkuu wa Polisi Gilbert Masengeli amehukumiwa kifungo cha miezi sita gerezani.
Katika uamuzi wake alioutoa leo Ijumaa, Jaji Lawrence Mugambi amemtaka Masengeli kujisalimisha kwa Kamishna Mkuu wa Magereza ili kutumikia kifungo hicho kama ilivyoagizwa na mahakama.
“Bw. Gilbert Masengeli amehukumiwa kifungo cha miezi sita jela. Bw. Masengeli ameagizwa kujisalimisha kwa Kamishna Mkuu wa Idara ya Magereza kuhakikisha anaanza kutumikia kifungo kilichotolewa dhidi yake gerezani,” amesema Jaji Mugambi katika uamuzi wake.
“Ikiwa hatajisalimisha kwa Kamishna Mkuu wa Magereza kama ilivyoagizwa, Waziri wa Usalama wa Kitaifa sharti achukue hatua zote zinazohitajika na zinazoruhusiwa kisheria kuhakikisha Bw. Gilbert Masengeli anatumikia kifungo chake gerezani alichohukumiwa.”
Jaji Mugambi amesema kifungo hicho kimetolewa kama agizo la kumshinikiza Masengeli wala siyo kumuadhibu.
Kwa misingi hiyo, Jaji huyo amesema amesitisha kutekelezwa kwa kifungo hicho kwa kipindi cha siku saba ili kumpa Masengeli fursa ya kufika mbele ya mahakama na kujibu mashtaka dhidi yake.
Aspofanya hivyo, kifungo hicho kitaanza kutekelezwa mara moja.
Masengeli mara kadhaa ametakiwa kufika mbele ya mahakama kuelezea waliko wanaharakati watatu wanaodaiwa kukamatwa na polisi wiki nne zilizopita.
Hata hivyo, hajaitikia wito huo na kumlazimu Jaji Mugambi kumhukumu kifungo hicho kwa misingi ya kuidharau mahakama.