Home Taifa Maseneta waikemea SRC kwa kupendekeza mshahara wa wabunge kuongezwa

Maseneta waikemea SRC kwa kupendekeza mshahara wa wabunge kuongezwa

0
kra

Mseneta wameikemea vikali Tume ya Mishahara na Marupurupu, SRC kwa kupendekeza kuongezwa kwa mishahara ya maafisa wakuu serikalini ikiwa ni pamoja na Maseneta, Wabunge, Mawaziri, Makatibu na Wawakilishi Wadi.

Maseneta hao wamemshutumu mwenyekiti wa SRC Lyn Mengich kwa kutaka kuongeza hamaki ya Wakenya hasa vijana wa Gen Z ambao wamekuwa wakifanya maandamano kulalamikia hali ngumu ya maisha nchini.

kra

“SRC inatafuta kuafikia nini kwa kupendekeza kuongeza mshahara wa maafisa wa serikali kwa wakati huu? SRC inawachochea Wakenya kuwa na chuki wakati huu ambapo nchi inakabiliwa na wakati mgumu,” alisema Seneta wa Kitui Enock Wambua katika bunge la Seneti leo Jumatano asubuhi wakati akichangia hoja ya hali ilivyo nchini kwa sasa.

Matamshi sawia yalitolewa na Seneta wa Nandi Samson Cherargei aliyetaka SRC kuvunjwa na makamishna wa tume hiyo kuhudumu kwa muda.

Cherargei aliliambia bunge la Seneti kuwa dhamira ya SRC ni kuchochea hamaki ya umma dhidi ya wabunge.

Ili kupunguza matumizi ya fedha za serikali, Seneta Wambua alipendekeza kupunguzwa kwa idadi ya mawaziri kutoka 21 hadi 14 na makatibu kutoka 51 hadi 30 au 14 ili kuhakikisha fedha nyingi zinaokolewa na kuelekezwa kwa maendeleo.

Seneta wa Kakamega Dkt. Boni Khalwale alipendekeza kuvunjwa kwa Baraza la Mawaziri na ofisi zisizokuwa za kikatiba kama vile Ofisi ya Mama Taif ana Kinara wa Mawaziri kufutliwa mbali.

Seneta wa Kericho Aaron Cheruiyot pia alitumia fursa hiyo kuilaani SRC na kusema kama Maseneta, wako radhi kupunguziwa mishahara yao ikiwa hatua hiyo itasaidia kuimarisha ukuaji wa uchumi na kukuza maendeleo ya nchi.

Ikiwa pendekezo la SRC la litatekelezwa katika Mwaka wa Fedha 2024/2025 ulioanza Julai Mosi mwaka huu, basi mshahara wa Maspika wa bunge la Taifa na Seneti utaongezwa hadi shilingi 1,208,362 kutoka shilingi 1,185,327, ya Mawaziri na Magavana itaongezwa hadi shilingi 990,000 kutoka shilingi 957,000 huku mshahara wa Naibu Spika ukiongezwa hadi shilingi 966,690 kutoka shilingi 948,261.

SRC pia imependekeza kuongezwa kwa mshahara wa Makatibu kutoka shilingi 792,519 hadi 819,844, viongozi wa walio wengi na wachache kutoka shilingi 784,768 hadi 800,019, Wabunge na Maseneta kutoka shilingi 725,502 hadi shilingi 739,600 huku tume hiyo ikipendekeza mshahara wa Wawakilishi Wadi kuongezwa kutoka shilingi 154,481 hadi shilingi 164,588.

 

 

Website | + posts