Gavana wa kaunti ya Meru Kawira Mwangaza kwa mara nyingine amejipata matatani baada ya wawakilishi wadi katika bunge la kaunti hiyo kupiga kura ya kumtimua madarakani.
Hii ni mara ya tatu kwa Gavana huyo kutimuliwa na bunge hilo, mara mbili akiwa alinusurika baada ya Bunge la Seneti kuingilia kati.
Katika kikao cha leo Alhamisi kilichojaa vurugu tele, wawakilishi wadi 49 walipiga kura ya kuunga mkono hoja ya kutimua madarakani wakati 17 wakiipiga.
Wawakilishi wadi watatu hawakupiga kura wakati wa kikao hicho kilichoshuhudia usalama ukiimarishwa maradufu nje na ndani ya majengo ya bunge.
Wakati huu, Mwangaza anakabiliwa na mashtaka ya ukiukaji wa katiba na sheria za kaunti, mienendo mibaya na utumiaji mbaya wa mamlaka yake.
Nadhari sasa ni kwa Bunge la Seneti kuona ikiwa kwa mara nyingine litamnsuru Gavana huyo ambaye amekuwa akilumbana na wawakilishi wadi tangu kuingia madarakani.