Home Habari Kuu Masaibu ya Mwangaza: Gavana wa Meru ataka Seneti kuingilia kati

Masaibu ya Mwangaza: Gavana wa Meru ataka Seneti kuingilia kati

0

Gavana wa kaunti ya Meru Kawira Mwangaza sasa analitaka bunge la Seneti kuingilia kati na kusuluhisha mzozo kati yake na Wawakilishi Wadi katika kaunti hiyo. 

Kupitia barua aliyomwandikia Spika Amason Kingi Oktoba 9, 2023, Gavana Mwangaza anaitaka Kamati ya Seneti inayoshughulikia Masuala ya Ugatuzi kuchukua jukumu la kusuluhisha mtafaruku kati ya pande hizo mbili ambao kwa muda mrefu umeathiri utoaji huduma katika kaunti hiyo.

“Naandika kukuarifu mzozo uliotokota ambao serikali yangu inakabiliana nao,” anasema Gavana Mwangaza katika barua hiyo.

Kulingana naye, aliridhiana na Wawakilishi Wadi baada ya jaribio lao la awali la kumtimua afisini kugonga mwamba, lakini katika siku za hivi maajuzi, tofauti kati yao zimechipuka tena.

Katika barua hiyo, Gavana Mwangaza anasema hana Wawakilishi Wadi mahususi wanaomuunga mkono kwani alichaguliwa kwenye wadhifa huo kama mgombeaji huru.

Katika kipindi ambacho amehudumu, anasema amekuwa akiwategemea Wawakilishi Wadi wa chama tawala cha UDA, lakini chama kimewaelekeza kutomuunga mkono kamwe.

“Septemba 23, 2023, chama cha UDA kiliitisha mkutano kupitia kiongozi wa wengi Evans Mawira na mwishoni mwa mkutano huo, waliwahutubia wanahabari na kuashiria kuwa wameondoa uungaji mkono wao kwa Gavana na kwamba hivi karibuni, watawasilisha hoja ya kunitimua kutokana na ‘kutomakinika kazini’,” alidai Gavana Mwangaza.

Anaongeza kuwa msimamo sawia ulichukuliwa na chama cha DEP, na kwamba Wawakilishi Wadi ambao wameelezea kumuunga mkono Gavana huyo wamekuwa wakitishiwa na kiranja wa wachache au wa wengi katika bunge la Meru.

“Hii imefikia kiwango kwamba baadhi ya Wawakilishi Wadi wameondolewa kutoka baadhi ya kamati za bunge,” anaongeza Gavana Mwangaza.

Anawanyoshea kidole cha lawama Naibu wake Isaac Mutuma, Seneta wa Meru Murungi Kathuri, Waziri wa Kilimo Mithika Linturi na wabunge kutoka kaunti hiyo anaosema wamekula njama ya kumhujumu.

“Kutokana na ari ya maridhiano na ikizingatiwa kuwa Kamati ya Seneti inayoangazia Masuala ya Ugatuzi ipo katika nafasi ya kutupatanisha kufuatia tofauti kati yangu, Naibu Gavana na bunge la Kaunti, nakuandikia nikiitaka kamati hiyo kuingilia kati,” anamalizia Gavana Mwangaza katika barua yake kwa Spika wa bunge la Seneti.

Wito ambao kamati hiyo imeitikia na imepangizwa kuzuru kaunti ya Meru wiki ijayo.

 

Website | + posts