Home Habari Kuu Maribe na Jowie sasa kujua hatima yao Machi 15

Maribe na Jowie sasa kujua hatima yao Machi 15

0

Hukumu dhidi ya mwanahabari Jackie Maribe na mpenziwe wa zamani Joshua Irungu, almaarufu Jowie, sasa itatolewa Machi 15, 2024.

Hukumu hiyo ambayo ni mara ya tatu kuahirishwa sasa ilitarajiwa kutolewa hii leo Ijumaa.

Hata hivyo, wakili wa Maribe, Katwa Kigen aliifahamisha mahakama kuwa mteja wake anaugua na ameenda hospitalini ili atibiwe.

Aliomba Maribe apewe siku saba za kupata nafuu.

Jaji Grace Nzioka ambaye alisikiliza kesi dhidi ya wawili hao alitaka ushahidi kuwasilishwa mahakamani kuthibitsha Maribe aliugua.

Jaji Nzioka ambaye ni Jaji Msimamizi wa Mahakama ya Naivasha alikuwa amesafiri kuja kutoa hukumu hiyo.

Maribe na Jowie wanashukiwa kuhusika katika mauaji ya mfanyabiashara Monicah Kimani mnamo mwaka 2018, mashtaka ambayo wameyakanusha.

Jowie ndiye mshukiwa mkuu huku Maribe akishtakiwa kwa kuwa msaidizi katika mauaji hayo.

Kesi hiyo ilikuwa iamuliwe mwezi Julai mwaka uliopita lakini uamuzi ukaahirishwa hadi Oktoba mwaka huo, kufuatia kuugua kwa jaji Nzioka.

Mashahidi 35 walitoa ushahidi wakati wa kusikilizwa kwa kesi hiyo.

Marehemu Kimani alipatikana ameuawa katika makao yake ya Lamuria Gardens, karibu na barabara ya Dennis Pritt mwaka 2018 mtaani Kilimani.