Home Habari Kuu Maribe na Jowie sasa kujua hatima yao kesho Ijumaa

Maribe na Jowie sasa kujua hatima yao kesho Ijumaa

0

Mwanahabari Jackie Maribe na mpenzi wake wa zamani Joshua Irungu, maarufu kama Jowie, sasa watajua hatima yao kesho Ijumaa, Februari 9, 2024 katika kesi ya mauaji ya mfanyabiashara Monica Kimani inayowakabili. 

Hukumu dhidi yao ilikuwa imepangwa kutolewa Machi 15, 2024 lakini timu za wanasheria katika kesi hiyo sasa zimeratibu upya tarehe ya kutolewa kwa hukumu hiyo.

Kulingana na timu hizo, hukumu hiyo, ambayo utoaji wake umeahirishwa mara tatu, sasa itatolewa kesho Ijumaa, Februari 9, 2024 kuanzia saa tatu asubuhi.

Kesi dhidi ya Maribe na Jowie ilisikilizwa na Jaji Grace Nzioka ambaye pia ni Jaji Msimamizi wa Mahakama ya Naivasha.

Jaji Nzioka alikuwa tayari kutoa hukumu hiyo Januari 26 mwaka huu lakini akafahamishwa kuwa Maribe ameugua.

Hii ilimlazimu kuahirisha utoaji wa hukumu hiyo hadi Machi 15 hadi uamuzi wa kusogezwa mbele kwa utoaji hukumu hiyo hadi Februari 9 kulipofikiwa.

Maribe na Jowie wanashukiwa kuhusika katika mauaji ya mfanyabiashara Monicah Kimani mnamo mwaka 2018, mashtaka ambayo wameyakanusha.

Jowie ndiye mshukiwa mkuu huku Maribe akishtakiwa kwa kuwa msaidizi katika mauaji hayo.

Kesi hiyo ilikuwa iamuliwe mwezi Julai mwaka uliopita lakini uamuzi ukaahirishwa hadi Oktoba mwaka huo, kufuatia kuugua kwa jaji Nzioka.

Mashahidi 35 walitoa ushahidi wakati wa kusikilizwa kwa kesi hiyo.

Marehemu Kimani alipatikana ameuawa katika makao yake ya Lamuria Gardens, karibu na barabara ya Dennis Pritt mwaka 2018 mtaani Kilimani.

Martin Mwanje & Ruth Wambui
+ posts