Home Kimataifa Marekani yatoa risasi milioni moja kwa Ukraine

Marekani yatoa risasi milioni moja kwa Ukraine

0

Marekani imetuma nchini Ukraine takriban risasi milioni 1.1 zilizonaswa kutoka Iran mwaka jana, jeshi lake limesema.

Kamandi Kuu ya Marekani (Centcom), ambayo inasimamia operesheni katika Mashariki ya Kati, inasema risasi hizo zilinaswa kutoka kwa meli iliyokuwa ikielekea Yemen mwezi Desemba.

Washirika wa Magharibi wa Ukraine hivi maajuzi walionya kwamba kampuni zao za uzalishaji zilikuwa zikijitahidi kuendana na kiwango ambacho Ukraine ilikuwa ikitumia risasi.

Centcom inasema risasi za Iran zilihamishwa hadi Ukraine Jumatatu wiki hii.

Awali, risasi hizo zilikamatwa na vikosi vya wanamaji vya Marekani kutoka kwa meli isiyo na uraia iitwayo MARWAN 1 mnamo tarehe 9 Disemba, ilisema.

Serikali ya Marekani ilipata umiliki wao mwezi Julai kupitia mchakato unaojulikana ambapo mali inaweza kutwaliwa ikiwa mmiliki wake anafikiriwa kuhusika katika shughuli za uhalifu.

Katika kesi hiyo, madai hayo yaliletwa dhidi ya Jeshi la Revolutionary Guard, tawi la jeshi la Iran lililopewa jukumu la kulinda serikali ya nchi hiyo.

Katika taarifa, Centcom ilisema Marekani “imejitolea kufanya kazi na washirika wetu kukabiliana na misaada inayosababisha vifo ya Iran katika kanda kwa njia zote halali”.

Iran inawaunga mkono waasi wa Houthi katika vita vya wenyewe kwa wenyewe vinavyoendelea Yemen, lakini uhamisho wa silaha kwa kundi hilo umezuiwa chini ya azimio la mwaka 2015 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.