Home Habari Kuu Marekani kuendelea kusaidia Ukraine hata inapokumbwa na matatizo ya bajeti

Marekani kuendelea kusaidia Ukraine hata inapokumbwa na matatizo ya bajeti

0
Rais Joe Biden. Picha/Hisani.

Rais wa Marekani Joe Biden ametangaza kwamba Marekani itaendelea kuisaidia Ukraine hata inapokumbwa na matatizo ya bajeti.

Haya yanajiri baada ya Biden kuonya bunge la Congress kwamba muda ulikuwa unayoyoma. Bunge hilo liliidhinisha ufadhili wa muda mfupi wa shughuli za serikali kuepusha hatari lakini likaondoa ufadhili wa Ukraine.

Ufadhili ambao Marekani inatoa kwa Ukraine ambayo iko kwenye vita na Russia unatarajiwa kuendelea hadi katikati ya mwezi Novemba tu.

Biden anaomba bunge kujadili na kuidhinisha ufadhili wa Ukraine haraka iwezekanavyo, kwani anaamini wabunge wengi wa pande zote za Democrat na Republican wanaunga mkono usaidizi kwa Ukraine ambayo ilivamiwa na Urusi.

Rais huyo alisihi viongozi hao waache michezo na watekeleze jukumu hilo akiongeza kwamba ana imani spika Kevin McCarthy wa chama cha Republican atahakikisha kwamba mswada tofauti umepitishwa wa kuidhinisha usaidizi wa kifedha kwa Ukraine.

Hata ingawa mswada uliopitishwa na bunge la Marekani Jumapili uliondoa ufadhili mwingine kwa Ukraine haijulikani kutatokea nini bungeni.

Biden na wanachama wa chama chake cha Democratic wanasema ni jukumu na Marekani kuisaidia Ukraine kujibu uvamizi wa Russia akisema iwapo watakosa kusaidia nchi hiyo, basi nchi nyingine zitapata ujasiri wa kutekeleza mashambulizi kama hayo katika nchi nyingine siku za usoni.

Suala la usaidizi kwa Ukraine limeingizwa siasa nchini Marekani jambo ambalo linatishia kukomesha usaidizi huo muhimu, Ukraine inapojikokota kujibu mashambulizi ya urusi kabla ya msimu wa baridi kuanza.

Website | + posts