Home Habari Kuu Marais Ruto na Biden wazungumza kwa njia ya simu

Marais Ruto na Biden wazungumza kwa njia ya simu

0

Rais William Ruto amefanya mazungumzo na Rais wa Marekani Joe Biden kwa njia ya simu. 

Wakati wa mazungumzo kati yao, Rais Ruto anasema walijadiliana kuhusiana na maadili ya pamoja ya kidemokrasia na kuheshimu utawala wa sheria kama jukwaa la kupanua fursa za kiuchumi na ustawi.

“Rais Biden aliishukuru Kenya kwa kukubali kuongoza misheni ya Usaidizi wa Usalama ya Nchi Nyingi (MSS) nchini Haiti na kuelezea kuwa Marekani inaunga mkono misheni hiyo. Pia aliipongeza Kenya kwa kufanikiwa kuwa mwenyeji wa Kongamano la Afrika kuhusu Tabia Nchi,” alisema Rais Ruto katika taarifa.

Kulingana na Rais Ruto, uhusiano kati ya Kenya na Marekani umeangazia upanuaji wa ustawi wa nchi hizo mbili.

“Tunaharakisha ukamilishaji wa makubaliano ya Ushirikiano wa Kimkakati wa Biashara na Uwekezaji (STIP), ambao utasaidia katika kuongeza biashara, kuongeza utengenezaji bidhaa, kubuni nafasi za ajira na kuongeza uwekezaji kati ya mataifa yetu,” aliongeza Rais Ruto.

Hususan, alisema uhusiano huo unalenga miundombinu, nishati mbadala, utengenezaji kijani wa bidhaa na kuwezesha biashara ndogondogo na za kiwango cha kati (MSMEs), ambazo ni nguzo muhimu katika ukuaji wa uchumi.

Rais Ruto ameahidi kuwa wataendelea kuangazia masuala ya usalama wa kikanda, utatuzi wa migogoro na vita dhidi ya ugaidi ili kuhakikisha Upembe wa Afrika una nafasi ya kushughulikia ustawi wa kijamii na kiuchumi.