Zaidi ya familia 100 zimeachwa bila makao, baada ya ardhi kuporomoka katika msitu wa Maasai Mau, kaunti ndogo ya Narok Kusini kutokana na mvua kubwa inayoendelea kunyesha kote nchini.
Akithibitisha kisa hicho naibu kamishna wa kaunti ndogo ya Narok Kusini Felix Kisalu, alisema mvua kubwa ambayo inashuhudiwa hapa nchini, imesababisha maporomoko mengi ya ardhi katika eneo hilo.
Aliongeza kuwa maporomoko hayo yalitokea katika kijiji cha Esongoroi kata ya Olashapani na kuacha zaidi ya familia 100 bila makao.
Hata hivyo Kisalu alisema hakuna maafa yoyote yaliyoripotiwa kufuatia maporomoko hayo.
Mtawala huyo alidokeza kuwa familia zilizoathiriwa zimehamishwa hadi maeneo salama, kama vile makanisa, shule na pia kwa majirani.