Home Michezo Man City waifunga Spurs 2-0 wakijizatiti kunyakua Ligi ya EPL

Man City waifunga Spurs 2-0 wakijizatiti kunyakua Ligi ya EPL

0
kiico

Mabingwa watetezi wa ligi ya Uingereza Manchester City wamezidi kuonyesha ubabe wa ligi hiyo Kwa kuilaza Tottenham Hotspur Kwa magoli mawili Kwa nunge kwenye mtanange wenye hisia Kali uliogaragazwa ugani White Hart Lane.

Timu zote zilionyesha kumakinika kipindi Cha kwanza hivyo kuishia sare ya nunge.Baada ya mapumuziko, vijana wa mkufunzi Pep Guardiola waliimarika na kupata bao namo dakika ya 51 kupitia Erling Haaland alipoandaliwa pasi nyerezi na Kevin De Bruyne.

Licha ya hali hii, Spurs hawakufa moyo kwani walinoa mashambulizi hadi kumujeruhi mlinda lango wa City Ederson alipogongwa na Pape Matar Sarr akiokoa mpira kwenye lango. Ederson aliondolewa uwanjani na kumpisha Stefan Ortega aliyemnyima Son Heung-min nafasi ya wazi kutinga goli.

Hata hivyo, kitumbua Cha Spurs kiliingia mchanga pale City walipozawadiwa mkwaju wa adhabu baada ya winga Jérémy Doku kuangushwa eneo hatari na kupelekea Haaland kutia wavuni bao la pili dakikia ya 91.

Kutokana na ushindi huo, City wanadedea kileleni mwa ligi Kwa alama 88 wakifuatwa na Arsenal Kwa alama 86 huku ukiwa umesalia mchuano mmoja ligi hiyo ikamilike. Mechi hiyo itasakatwa jumapili hii saa 18:00.

Iwapo Wana City watashinda West Ham Ugani Etihad, watakuwa timu ya kwanza kunyakua taji hilo mara nne mtawalia. Na iwapo watashindwa nao Arsenal washinde Everton pale Emirates, basi Arsenal watatawazwa washindi Kwa muda wa miaka 19. Nayo sare ya nunge Kwa City bado itawapa Arsenal ubingwa kupitia wingi wa mabao.

kiico