Mama ya mwanamuziki Mr. Seed alizikwa jana Jumamosi Septemba 14, 2024 nyumbani kwao huko Siaya.
Mzazi huyo wa Mr. seed amekuwa akiugua kwa muda wa miaka miwili kutokana na kile alichokitaja kuwa tatizo la uti wa mgongo alilopata baada ya kuanguka.
Seed alielezea kwamba tangu wakati huo, mamake amekuwa akiishi na uchungu kwani aliambiwa na madaktari kwamba kuna diski ilikuwa imeumia kwenye uti wa mgongo na hata upasuaji wa kuirekebisha ulikuwa hatari kwa maisha yake.
Siku ambayo mamake alikata roho, Seed anasema alikwenda kumwona hospitali jioni, akamwomba maziwa mala. Seed anasema alinunua maziwa hayo akampa kisha akaenda nyumbani.
“Nilipatwa na hisia za kuogofya usiku huo. Nikalazimika kuzima simu ndiposa nilale.” Alisema Seed akiongeza kwamba alipoamka asubuhi na kuwasha simu, alipigiwa na madaktari waliomfahamisha kwamba mamake ameaga dunia.
“Nilienda nikamwona. Alikuwa amelala kwa amani.” aliongeza mwanamuziki huyo.
Akizungumza wakati wa ibada ya kumuaga mamake Seed katika kanisa la KAG Mirema, mwanamuziki mwenza Jaguar alielezea jinsi aliamua kumsaidia mama huyo kupata matibabu.
Anasema punde baada ya kufahamishwa kuhusu hali yake, alishauri familia yake impeleke kwenye hospitali moja inayomilikiwa na rafiki yake kwenye barabara ya Ngong jijini Nairobi.
Mara ya mwisho Jaguar alimzuru mama huyo hospitalini, alikuwa anajiandaa kwa upasuaji kesho yake ambapo alimhimiza ale vizuri.
Jaaguar anasema kesho yake alipigiwa simu kufahamishwa kwamba upasuaji haukwenda vizuri na mgonjwa alikata roho.
Mazishi ya mama huyo yalihudhuriwa na wanamuziki kadhaa mashuhuri humu nchini akiwemo Bahati.