Mkewe Rais, Mama Taifa Rachel Ruto amezindua vifaa vya matibabu ambavyo vitafaidi kaunti za maeneo kame humu nchini.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa vifaa hivyo katika ikulu ya Nairobi, Bi. Rachel alisema kwamba baadhi ya kaunti zinazolengwa ni Baringo, Samburu na Marsabit.
Alisema kutopatikana kwa huduma za afya ni mojawapo ya changamoto kubwa katika kujenga taifa lenye afya, akielezea kwamba lengo la vifaa hivyo ni kupeleka huduma za afya karibu na watu.
Vifaa vilivyozinduliwa leo ni pamoja na kliniki za magari zenye vifaa hitajika vya kutoa chanjo, friji na magari yaliyo na friji ya usafirishaji dawa.
“Vifaa hivi vitahakikisha kwamba dawa na chanjo zinasalia kuwa nzuri kwa matumizi ya binadamu, hasa katika mazingira ya maeneo hayo.” alisema mama Rachel Ruto.
Mkewe Rais alishukuru washirika waliowezesha upatikanaji wa vifaa hivyo kama benki ya maendeleo ya Ujerumani na hospitali ya chuo kikuu cha Aga Khan.
Alisema hatua hiyo inawiana na kujitolea kwa serikali kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora za afya kwa wote almaarufu “universal health coverage” nguzo muhimu ya mpango wa uwezeshaji wa serikali ya Kenya Kwanza kwa jina “Bottom-Up Economic Transformation Agenda”.
Waziri wa Afya Susan Nakhumicha, mwenyekiti wa kamati ya afya katika baraza la mawaziri Muthomi Njuki na viongozi wa kaunti zinazolengwa walihudhuria hafla ya uzinduzi wa vifaa hivyo.