Mama Taifa Rachel Ruto aongoza sherehe za miaka 14 ya JOYWO

Marion Bosire
2 Min Read
Mama Taifa Rachel Ruto akiwasili Kasarani

Mama Taifa Rachel Ruto hivi leo anaongoza sherehe za kuadhimisha miaka 14 ya uwepo wa shirika la wanawake la JOYWO katika ukumbi wa uwanja wa michezo wa Kasarani.

Sherehe hizo zinahudhuriwa na wake kadhaa wa marais barani Afrika kama vile Monica Geingos mke wa rais wa Namibia, Rebecca Akufo-Addo, mkewe Rais wa Ghana na Angeline Ndayishimiye, mkewe Rais wa Burundi.

Shirika la wanawake la Joyful Women Organisation, JOYWO lilibuniwa na Mama Rachel Ruto kwa lengo la kuwapa wanawake uwezo kiuchumi ambapo walihitajika kubuni makundi, kutoa michango yao na kupata mikopo ya kufanya biashara kutoka kwa makundi hayo.

Wanawake wapatao elfu 20, kutoka kaunti 44 nchini wamejumuika huko Kasarani kwa sherehe za leo.

Kulingana na takwimu kwenye tovuti ya shirika hilo, shirika la JOYWO lina wanachama wapatao elfu 188 kote nchini ambao wako kwenye makundi zaidi ya elfu 15.

Pesa ambazo zinazunguka katika shirika hilo kwa sasa ni dola milioni 21 sawa na bilioni 3.2 pesa za Kenya.

Kila mwanachama wa shirika hilo ana fursa ya kupata mkopo wa hadi mara tatu ya pesa alizowekeza kama hisa na muda wa kurudisha huwa kati ya mwaka mmoja na miaka miwili.

Baadaye, wake wa Marais barani Afrika kupitia shirika lao la “Organisation of African First Ladies for Development – OAFLAD” ambalo kwa sasa linaongozwa na Rebecca Akufo-Addo, wanatarajiwa pia kuzindua kampeni ya kuunganisha Kenya.

Website |  + posts
Share This Article