Home Burudani Mama Onyeka Onwenu afariki

Mama Onyeka Onwenu afariki

0
kra

Mwimbaji, mwigizaji na mwanaharakati wa Nigeria Mama Onyeka Onwenu ameaga dunia. Onwenu ambaye aliwahi pia kuwa mtangazaji amefariki akiwa na umri wa miaka 72.

Inaripotiwa kwamba alimaliza kutumbuiza kwenye hafla moja jana Jumanne usiku jijini Lagos nchini Nigeria na kugonjeka. Saa chache baadaye alifariki akipokea matibabu katika hospitali moja iliyo karibu.

kra

Miaka ya 1980, Onyeka alitumia fani zake mbali mbali kutetea haki za wanawake hatua ambayo ilisababisha apatiwe jina la “Elegant Stallion”.

Rais wa Nigeria Bola Tinubu ameongoza viongozi na wananchi wa taifa hilo kumwomboleza Onyeka akisema kwamba ataishi milele kupitia kazi zake za sanaa.

Anafahamika sana kwa kibao alichotoa mwaka 1986 kiitwacho “One Love” na kingine “You and I” kilichorekodiwa upya na kutumiwa kwenye filamu ya “Conspiracy” ya mwaka 1999 ambayo aliigiza.

Onyeka Onwenu ni mzaliwa wa eneo la Obosi jimbo la Anambra na alizaliwa Januari 1952.

Babake kwa jina Dickson Onwenu alikuwa mwanasiasa hata kabla ya nchi hiyo kujipatia uhuru na mamake kwa jina Hope Onwenu alikuwa mwimbaji.

Alikwenda Marekani kwa elimu ya juu ambapo alisomea katika taasisi za Wellesley College iliyoko Massachusetts na New School iliyoko New York.

Punde baada ya kurejea nchini Nigeria, Onyeka aliingilia muziki na utangazaji katika chumba cha habari kinachomilikiwa na serikali ya Nigeria.

Aliandika na kusimulia makala ya “Nigeria: A Squandering of Riches” ya mwaka 1984 yaliyoandaliwa kwa ushirikiano kati ya chumba hicho cha utangazaji cha serikali na shirika la utangazaji la Uingereza BBC.

Mama huyo aliigiza kwenye filamu kadhaa za Nigeria.

Anafahamika kwa kutetea na kutafuta kuachiliwa kwa mwanamuziki mwenza Fela Aníkúlápó Kútì na katika kitabu alichoandika mwaka 2021 alielezea kwamba baada ya kuachiliwa Kuti alitaka kumwoa.

Onwenu alikataa ombi la Kuti kwani alikuwa tayari ameoa wake wengi naye alijifahamu kwamba ana wivu na hangeweza kung’ang’ania mapenzi yake.

Alirekodi albamu nne za nyimbo za kidunia kabla ya kuokoka na kuanza kuimba nyimbo za injili miaka ya 1990.

Ameacha watoto wawili wa kiume aliobarikiwa nao akiwa kwenye ndoa lakini baadaye alitoka kwenye ndoa akitaja msongo wa mawazo na kuamua kulea wanawe peke yake.

Website | + posts