Home Habari Kuu Mali yakatiza uhusiano wa kidiplomasia na Ukraine

Mali yakatiza uhusiano wa kidiplomasia na Ukraine

0
kra

Taifa la magharibi mwa Afrika la Mali limetangaza kwamba limekatiza uhusiano wa kidiplomasia na Ukraine likilaumu afisa mmoja mkuu wa Ukraine kwa kukubali kwamba nchi hiyo ilihusika na ushinde wa Julai.

Shambulizi hilo linasemekana kusababisha vifo vya mamluki 84 wa kundi la Wagner kutoka Russia pamoja na wanajeshi 47 wa Mali, katika vita vya siku tatu kaskazini mwa Mali.

kra

Huo ndio ushinde mkubwa kabisa wa kundi la wagner tangu lilipoingilia vita nchini Mali miaka miwili iliyopita.

Andriy Yusov msemaji wa kitengo cha ujasusi cha jeshi la Ukraine aliambia shirika la utangazaji la Suspilne mnamo Julai 29, 2024 kwamba waasi nchini Mali walikuwa wamepokea habari zote walizohitaji zilizowawezesha kutekeleza oparesheni dhidi ya wahalifu wa vita wa Russia.

Mali inasema ilifahamu kwa masikitiko makubwa matamshi ya Yusov na kwamba alikuwa amekubali kuhusika kwa Ukraine katika shambulizi lililotekelezwa na waasi na kusababisha vifo vya wanajeshi.

Taarifa ya msemaji wa serikali ya Mali Kanali Abdoulaye Maiga inaelezea kwamba uhusiano kati ya Ukraine na Mali unakatizwa mara moja.

Mali ilitaja pia matamshi ya balozi wa Ukraine nchini Senegal Yurii Pyvovarov, aliyeitwa na serikali ya nchi hiyo Jumamosi kuelezea aliyoyasema kwenye video iliyosambazwa mitandaoni.

Kwenye video hiyo, Pyvovarov alisikika akiunga mkono kikamilifu shambulizi hilo la waasi.

Kulingana na Maiga, vitendo vya Ukraine vinakiuka uhuru wa Mali na ni mwingilio usiokubalika na uungaji mkono wa ugaidi wa kimataifa.

Mapigano makali ya siku tatu yalizuka nchini Mali karibu na mpaka wa Algeria Julai 25 katika kambi ya wanajeshi ya Tinzaouatene.

Waziri wa masuala ya kigeni wa Russia Sergey Lavrov ametoa hakikisho la kuendelea kuunga mkono Mali katika mazungumzo ya simu na mwenzake wa Mali Abdoulaye Diop.

Website | + posts