Home Habari Kuu Makatibu watuzwa kwa utendakazi mwema

Makatibu watuzwa kwa utendakazi mwema

0

Taasisi ya Makatibu walioidhinishwa (ICS) imeahidi kuendelea kutambua watu binafsi na taasisi zilizopiga hatua katika kukuza uadilifu na utawala bora.

Mwenyekiti wa taasisi hiyo, Joshua Wambua, amesema taasisi ya ICS itatambua na kutuza watu ambao wamekabili changamoto na vikwazo na wakaweza kufanikiwa katika kudumisha kanuni za utawala bora katika utekelezaji wa majukumu yao katika sekta za umma na kibinafsi.

Akizungumza kwenye hafla ya kutoa tuzo kwa wanachama 11 wa taasisi hiyo na kuwavisha taji ya heshima watu watatu wasio wanachama, Wambua alisema kila tuzo inayotolewa inaashiria imani kwa uwezo wa watu binafsi na mashirika katika kuleta mabadiliko katika jamii.

Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya mafuta ya Bidco, Vimal Shah, ambaye aliongoza hafla hiyo alitoa changamoto kwa viongozi wa mashirika mbalimbali kuwa mstari wa mbele katika vita dhidi ya ufisadi ili kuwa mfano bora kwa wafanyakazi walio chini yao na hivyo kukomesha kero hilo ambalo limefilisisha kampuni nyingi ambazo awali zilikuwa zikinawiri.

Mwenyekiti wa tume ya kupambana na ufisadi humu nchini David Oginde, katibu katika wizara ya fedha Chris Kiptoo na afisa mkuu mtendaji wa tume ya utumishi wa umma Dk Simon Rotich, walituzwa licha ya kutokuwa wanachama wa taasisi ya ICS.

Rotich alisema tuzo hizo ni utambuzi wa kazi nzuri ambayo tume ya utumishi wa umma inafanya katika kukuza uadilifu katika sekta hiyo.

Wanachama wa taasisi ya ICS ambao wamehudumu kwa muda mrefu, Rebecca Miano ambaye ni waziri wa viwanda na biashara pamoja na katibu wa baraza la mawaziri Nancy Wanjau pia walituzwa.